Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
alitoa msimamo huo jana baada ya Spika Makinda kueleza bungeni kuwa
Lissu ndiye kinara wa vurugu, huku ikielezwa kuwa Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge itamchukulia hatua za kinidhamu.Kabla ya Spika Makinda kuahirisha Bunge, kulitokea mvutano kati
yake na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari baada ya
Makinda kumweleza kuwa hajui kanuni hivyo atulie.
Hata hivyo, alimruhusu kuzungumza na ndipo
Nassari alipopinga Kamati ya Uongozi ya Bunge kufuta hoja binafsi za
wabunge akieleza ni kinyume cha kanuni za Bunge kufanyika kitu hicho.
Kabla ya Spika Makinda kujibu, Lissu alisimama
na kuomba mwongozo wa Spika akisema; “Mheshimiwa Spika tunataka
utueleze tutaendelea kukata rufaa hadi lini, wakati una rufaa zetu 10
kuanzia mwaka juzi na hujazitolea uamuzi, naomba mwongozo wako
Mheshimiwa Spika,” alisema Lissu na kujibiwa na Spika Makinda kuwa,
“Rufaa hizo zinafanyiwa kazi na zitatolewa uamuzi.”
Makinda aliliahirisha Bunge kwa kile
alichosema kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu ndani ya Bunge
hilo na kufuta hoja binafsi ambazo hutolewa na kuchangiwa baada ya
kipindi cha maswali na majibu.
Makinda alisema: “Waheshimiwa wabunge, tangu
Januari 30, hadi jana (juzi) Februari 4, 2013 tuliamua kuwasilisha
bungeni hoja binafsi za wabunge ambazo ziliahirishwa katika mkutano wa
tisa wa Bunge kwa nia njema ya kujadiliana masuala makubwa ya kitaifa na
kuishauri Serikali nini kifanyike ili kukabiliana na matatizo
mbalimbali yanayowahusu wananchi.
“Hata hivyo, imelazimu kuahirisha mijadala
yote ya hoja binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu
kwa baadhi ya wabunge na hivyo kuamua kwa makusudi kuanzisha vurugu na
kulifanya Bunge kupoteza heshima yake,” alisema Spika Makinda.
Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya
Uongozi imekubaliana kuwa suala hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge ili ilichunguze na kuwasilisha mapendekezo
yake kabla ya mkutano unaoendelea kumalizika na kwamba hoja zote binafsi
zisiwasilishwe kutokana na utovu wa nidhamu ambao ungeweza kujitokeza
katika hoja zilizobakia.
Hata hivyo, Lissu alisema kuwa kelele za kutetea taratibu na kanuni ndizo zinamfanya aonekane kuwa ana utovu wa nidhamu.
“Spika anaonyesha upendeleo wa waziwazi,
anakiuka kanuni kwa makusudi. Mimi nitasema, sitaogopa kamati, hata
nikiitwa nitasema... Sasa tunachokifanya, tumekutana leo (jana) na
tumeandaa taarifa ya kutaka Spika aondolewe yeye na naibu wake, hii
tutaiwasilisha kama taarifa kati ya kesho (leo) na keshokutwa (kesho),”
alisema Lissu.
0 Comments