Mwanafunzi wa chuo cha ufundi akirekebisha Kompyuta.
KILA mwaka, zaidi ya nusu ya wanafunzi wanaohitimu darasa la
saba na kidato cha nne, hawapati fursa ya kuendelea na ngazi ya elimu
iliyo mbele yao kwa sababu mbalimbali.
Mfano mzuri ni mwaka jana ambapo wanafunzi
waliofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba walikuwa 983, 545, lakini
waliofaulu ni 567,567. Hivyo wanafunzi 415,978 hawakufanikiwa kuendelea
na masomo ya sekondari.
Katika kundi hili wamo watakaosomeshwa na wazazi,
walezi ama wafadhili katika shule binafsi. Lakini kuna maelefu wengine
watakwama kabisa kuendelea na elimu ya sekondari.
Kwa nchi masikini kama Tanzania, kuzalisha watu zaidi ya 500,000 kila mwaka ambao hawapati ujuzi wowote, ni kuongeza umaskini katika nchi
ambayo hivi karibuni tulielezwa kuwa idadi ya watu wake imefika milioni
44.
Hili ni doa kubwa katika mchakato wa kuiletea nchi
maendeleo. Makala haya yanauliza kwa mwenendo huu, ni lini Tanzania
inaweza kuifikia nchi kama vile Korea Kusini ambayo mpaka mwaka 1961
ilipopata uhuru, viwango vya uchumi vya nchi mbili hizo vilikuwa
vinalingana.
Naibu Spika wa Bunge la Korea Kusini, Park
Byeong-Seug, anasema mwanzoni nchi yake ilikuwa kama Tanzania, na wala
haikuwa na maliasili ambazo zingeweza kuikwamua.
Kutokana na hali hiyo, anasema kuwa waliamua kuwekeza kwenye rasilimali watu na hiyo ndiyo siri ya mafanikio yao.
“Korea hatukuwa na maliasili, tuliwekeza kwa watu.
Kuwekeza kwenye akili ndiyo siri ya mafanikio yetu. Elimu ndiyo siri
kubwa kama unataka kupata maendeleo,” anafafanua.
Tofauti na Korea Kusini, Tanzania imejaaliwa
rasilimali za kila aina kama madini, wanyama, gesi, ardhi, misitu na
nyingine nyingi, lakini bado wananchi wengi wanaishi katika maisha ya
kifukara.
Ujenzi wa vyuo vya ufundi
Kwa baadhi ya watu kiwango hicho cha umaskini
kingeweza kupungua endapo nchi ingekuwa na vyuo vingi vya ufundi stadi
ambavyo kazi yake ingekuwa kuhakikisha kila mhitimu wa darasa la saba na
kidato cha nne anayeshindwa kuendelea na masomo ya juu, anapatiwa stadi
za kumwezesha kujitegemea.
Kwa kufanya hivi, vijana ambao sasa wanaonekana mitaani wakiwa hawana cha kufanya, wangepata ujuzi ambao ungewasaidia kujiajiri.
|
0 Comments