VIONGOZI na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walifanya maandamano na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara uliofanyika Temeke, jijini Dar es Salaam ambako chama hicho kilitangaza nia ya kuandaa hoja ya kuwang’oa viongozi wa Bunge.
Hoja hiyo itawasilishwa katika mkutano ujao wa Bunge kwa ajili ya kuwapigia kura za kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kwa madai ya kukwamisha mijadala yenye masilahi ya wananchi bungeni.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Temeke Mwisho, Dar es Salaam, wabunge wa chama hicho wakiwa na uongozi wa juu, waliwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo kujiandaa na maandamano ya kuwang’oa spika hao.Kana kwamba hiyo haitoshi, wabunge hao walitangaza namba za simu za viongozi hao wa Bunge ili wananchi wazitumie kuwashinikiza wang’oke.
Akihutubia katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe alisema Spika Makinda ameshindwa kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (Epa).
Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia masilahi ya wananchi.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Zitto alitaja mbinu za kumng’oa Spika Makinda akisema kuwa hoja hiyo imeshakamilika.
“Kuna njia za kumng’oa Spika Makinda, kwanza kwa kupeleka hoja ya kutokuwa na imani naye na nimeambiwa hapa kwamba imeshakamilika. Au tuandamane hadi pale Shule ya Msingi Bunge… au tutumie namba zake kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…” alisema Zitto na kumruhusu Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kutaja namba za Spika Makinda na Naibu wake.
Baada ya kutaja namba hizo wananchi walionekana wakizipiga na wengine kutuma ujumbe wa simu.
Mwananchi lilipompigia simu Spika Makinda, simu yake ilikuwa inaita, kisha inakatika bila kupokewa.
Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto alisema:
“Kamati hii iliundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Spika Samuel Sitta kwa ushauri wa kina Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu Chadema), waliona kuwa haiwezekani nchi yenye zaidi ya mashirika 200 yenye thamani ya zaidi ya Sh10 trilioni yasidhibitiwe na Bunge…Lakini Serikali ya CCM ikaona upinzani umepata sehemu ya kuzungumzia, sasa wameifuta,” alisema Zitto.
Alitaja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo Kikuu cha Arusha.