Mapigano baina ya wanajeshi wa serikali ya Mali na wapiganaji wa
Kiislamu kwa mara ya kwanza yamefika kati-kati ya mji wa Gao, mji mkubwa
kabisa kaskazini mwa nchi.Mwandishi wa BBC alioko huko anasema wanajeshi wa Ufaransa wanatumia mizinga dhidi ya wapiganaji hao walioingia hapo kabla.
Anasema ghasia zilianza karibu na makao makuu ya polisi, lakini mapigano yametapakaa.
Wanajeshi wa Ufaransa na Mali waliukomboa mji huo mwezi uliopita.
Shirika la habari la Ufaransa linaeleza kuwa
wapiganaji wa Kiislamu waliovaa nguo nyeusi, huku wamebeba bunduki,
waliteka eneo la kati ya mji wa Gao, mji wenye wakaazi wengi kabisa
kaskazini mwa Mali.
Wapiganaji hao walipambana na wanajeshi wa Mali
leo jioni kwa zaidi ya saa mbili na walionekana wakiranda mitaani kwa
pikipiki na wengine walikuwa juu ya mapaa karibu na makao makuu ya
polisi.
Karibu na makao hayo wanajeshi wa Mali walitumia
makombora na kupambana kwa risasi na washambuliaji ambao wanafikiriwa
kuwa wafuasi wa kundi la MUJAO, linalodai kupigana jihadi Afrika
Magharibi.
Sauti zilizosikika ni risasi na mbuzi wakikimbia huku wakaazi wa mji wamejificha majumbwani mwao.
Tangu wanajeshi wa Ufaransa kuukomboa mji wa
Gao, wapiganaji wa Kiislamu walipambana na wanajeshi nje ya mji lakini
hii ndio mara ya kwanza wamefanikiwa kuingia ndani ya mji. |
0 Comments