RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)kuhakikisha inaendesha zoezi la utambuzi wa watu kwa uhakika na makini akisema kuwa, hali yoyote itayosababisha kutolewa kwa vitambulisho katika mazingira ya ujanja inaweza kuwagharimu watumishi wa mamlaka hiyo.

Kwa upande mwingine, Rais Kikwete jana alikabidhiwa rasmi kitambulisho chake cha taifa na hivyo kuwa miongoni mwa Watanzania wa kwanza kukabidhiwa. Wengine waliokabidhiwa vitambulisho vyao ni pamoja marais wastaafu wa awamu ya pili na ile ya tatu, Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mfumo wa usajili na utambuzi kwa wa watu na utoaji vitambulisho vya taifa, Rais Kikwete alionya juu ya utoaji vitambulisho kwa watu wasiostahili na kusema kwamba Serikali yake haitavumilia kuona hali hiyo ikitendeka.
Alisema suala la vitambulisho vya taifa ni nyeti na linapaswa kuendeshwa kwa kufuata miiko na sheria za nchi, hasa kwa kuzingatia kuwa vitambulisho hivyo vitatumika wakati wa uchaguizi mkuu ujao.

“ Katika hili sitakuwa na mswalie mtume, maana kama kuswalia tulifanya hivyo kabla ya kuwapatia kazi hii. Nataka muendeshe mambo kwa kuzingatia miiko na sheria, sitaki kuona mtu asiye raia wa Tanzania halafu anapatiwa kitambulisho cha uraia.” Alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa .

“ Yale tunayoyashuhudia kwenye uhamiaji, sitaka yajitokeze tena huku maana siku hizi ‘passport’ yetu (hati ya kusafiria) inatolewa ovyo ovyo mitaani”
Kuanza kutolewa kwa vitambulisho hivyo vya taifa, kunakamilisha ndoto ya miaka mingi iliyoasisiwa wakati wa utawala wa awamu ya kwanza na baadaye kuendelea hadi awamu hii ya nne.

Vitambulisho vya taifa vinatazamiwa kusaidia maeneo ya ulinzi na usalama, kutumika kama kitambulisho rasmi wakati wa uchaguzi mkuu ujao na pia kutumiwa kama vyanzo rahisi vya upataji taarifa kwa taasisi za kifedha ikiwamo benki.

Kama sehemu ya kuimarisha utendaji kazi, mamlaka hiyo ya vitambulisho vya taifa imeanzisha ushirikiano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec),ambayo inakusudia kuvitumia vitambulisho hivyo katika uchaguzi mkuu ujao. Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu alisema ushirikiano huo itasaidia kuboresha kazi za utoaji vitambulisho na kwamba utakamilika kwa wakati. Hata hivyo alisema bado ofisi yake inakabiliwa na tatizo la vitendea kazi na kuiomba serikali kuongeza bajeti.

Hadi sasa mamlaka hiyo imekamilisha kukusanya taarifa kutoka kwa wakazi wa Dar es salaam na ilipanga kuendelea na zoezi hilo katika mikoa mingine.Ili kupata kitambulisho hicho wananchi wanapaswa kuwasilisha taarifa zao kupitia fomu maalumu zinazosambazwa na mamlaka hiyo na baadaye kuchukuliwa kwa alama za vidole, picha na saini za kielekroniki.

Vitambulisho hivyo vitaanza hivi karibuni kutolewa kwa watumishi wa umma, kwani taarifa zao pamoja na alama nyingine zilikwisha chukuliwa. Hatua hiyo inakuja katika wakati ambapo taifa liko kwenye mchakato wa uandikwaji wa katiba mpya, ambayo nayo pia imepangwa kupatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Kuhusu Zanzibar ambayo inatumia vitambulisho vya mkazi vilivyoanza kutumika tangu mwaka 2006, kumeelezwa kuwa, wananchi wa eneo hilo nao watajumuishwa kwenye zoezi hilo.