INAKISIWA kuwa katika kila dakika moja, watoto wa kike 19 wenye umri chini ya miaka 18 wanaolewa kwa nguvu duniani.
Kuwa mtoto wa kike katika nchi zinazoendelea katika Bara la Asia (asilimia 46) na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (asilimia 38) ni mbaya zaidi kutokana na kukithiri kwa ndoa za mapema na za kulazimishwa.
Kwa mujibu wa shirika la kimaitaifa la kuchangia maendeleo ya watoto (PLAN) wasichana zaidi ya millioni 14 wanaolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Nchi za Chad, Niger, na Mali zinaongoza!
Hata hivyo inawezekana kuwa Zanzibar, nchi yenye wakazi zaidi ya milioni moja, na wenye kufuata utamaduni wa Kiislamu ni miongoni mwa nchi zilizokuwa na idadi kubwa ya wasichana wanaolazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo.
Utafiti uliyofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) umeonesha kuwepo kwa tatizo la kuwalazimisha wanafunzi kuolewa mapema visiwani Zanzibar, mjini na vijijini, hata hivyo, ripoti ya utafiti huo umebaini kuwa takwimu zilizopatikana ni chache kulinganisha na hali halisi kutokana na kuwa ndoa nyingi za kulazimishwa hazifikishwi katika vyombo vya sheria.
Kwa jumla takwimu za Wizara ya Elimu, ni kesi 32 za kulazimishwa kuolewa zilirekodiwa mwaka 2011, na kwamba kesi nyingi hazifikishwi polisi isipokuwa wanafamilia husuluhishana wenyewe kwa wenyewe na kwa wale wanaokataa suluhu ndiyo wanaofikishana polisi na mahakamani.
Baadhi ya watu waliohojiwa katika utafiti wa TAMWA, walieleza kuwa ndoa za kulazimishwa zinaendelea kutokana na kulazimishwa au mimba za utotoni kwa wanafunzi.
Baadhi ya mifano ya ndoa za kulazimishwa ni Wilaya ya Micheweni, Pemba ambako kwa wastani wanafunzi kumi (10) hukatishwa masomo na kuolewa katika skuli za Tumbe na Micheweni kila mwaka.
Wilaya ya Magharibi, Unguja- mwaka 2011 jumla ya kesi 13 za wanafunzi kupata mimba zilipelekwa Wizara ya Elimu kwa uchunguzi ambapo baadhi yao waliolewa.
Wilaya ya Kaskazini A, Unguja- tatizo la watoto wa kike kukatishwa masomo na kuolewa lipo kwa kiasi kikubwa katika Wilaya ya Kaskazini “A” Mkuu wa Wilaya, Riziki Juma Simai alisema tatizo hilo lipo lakini hakuna anaekwenda kuripoti au kushtaki kwa sababu inapotokea mwanafunzi kubeba mimba wazazi wanachukua uamuzi wa kumuoza.
“Iwapo wao viongozi wa wilaya wanapata taarifa basi harusi zinavunjwa, ili mtoto wa kike aendelee na masomo, na hii inakuja iwapo anayeolewa hana mimba na mwenyewe anataka kuendelea na masomo,” anasema Simai
Anaongeza: “Tuna tatizo kwa sababu wazee wanachukua uamuzi wa kufanya harusi wenyewe na Serikali ikiingilia basi unaona harusi inafanywa haraka haraka lakini hata hivyo tunapopata habari tu tunachukua hatua za kuivunja hiyo harusi lakini wakati mwingine wazee wanakuwa na ukaidi sana”