MAELFU ya wakazi wa Jiji la Arusha ,wakiwamo maaskofu, wanasiasa
jana walifurika katika mazishi ya Askofu Dk Thomas Laiser wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri(KKKT) Dayosisi ya Mjini Kati, wakiongozwa na Rais
Jakaya Kikwete.
Wengine waliohudhuria ni Marais wastaafu,
Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa,
mawaziri kadhaa, wabunge na viongozi wengine ndani na nje ya nchi.
Mazishi ya aina yake ya Askofu Laizer aliyefariki Februari 7, mwaka huu
katika Hospitali ya Selian kutokana na kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa
saratani, yalisababisha barabara kadhaa kufungwa Arusha na yalifanyika
katika kanisa la Mjini Kati.Mazishi ya askofu huyo yalitanguliwa na zoezi la kuaga mwili, lililoanza juzi kanisani hapo. Akizungumza
katika ibada ya mazishi ya Askofu Laiser, Rais Jakaya Kikwete alisifu
kazi nzuri ambazo amezifanya katika sekta ya elimu, afya na huduma za
jamii.
“Aliyofanya Laizer yanajieleza yenyewe kama
ujenzi wa shule, zahanati, vituo vya afya miradi na maji, vyote hivi
vimepatikana kwa juhudi zake kwa manufaa ya dayosisi kwani askafu huyu
alikuwa mpenda watu,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema njia nzuri ya kumuenzi
Askofu Laizer ni katika mazingira ambayo nchi inapitia kwa sasa ni vyema
kujenga msingi watu kuishi kwa umoja na mshikamano bila kujali dini,
kabila wala rangi zao.
“Katika kumuenzi tujiepushe kufanya mambo ambayo yatapandikiza chuki katika jamii hata kama ukichukizwa kiasi gani,” alisema.
Alisema huu ni wakati wakujikusanya siyo
kujitenga, tusifanye mambo ambayo yatapandikiza uhasama au ugomvi baina
ya watu ni vyema kuhimiza watu kuishi pamoja kwa upendo na amani licha
ya tofauti za kidini. Rais Kikwete alisema alimfahamu Askofu Laiser
tangu alipokuwa waziri na ameshirikiana naye katika mambo mengi ya
kimaendeleo, kwani ni mtu ambaye aliishi kwa upendo na kuhimiza amani.Kwa niaba ya Serikali Rais Kikwete alitoa pole kwa familia ya
Laizer, Kanisa la KKKT na waumini wote wa kanisa hilo, kwa kuondokewa na
Askofu wao mpendwa. Mbowe,Mbatia na Sendeka watoa kauli nzito .
Katika ibada hiyo, pia walihudhuria viongozi
wa kisiasa na wa kwanza kuzungumza alikuwa Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe ambaye alieleza uhusiano wake na marehemu Askofu Laizer ya
muda mrefu.
“Askofu Laiser alikuwa mtu wangu wa karibu
sana, ni yeye ndiye aliongoza sherehe yangu ya kufikisha miaka 50,
ambapo pia mimi nilikuwa ni kati ya watu wa mwisho wa maisha yake
kukutana naye,” alisema Mbowe.
Alisema kauli ya mwisho ambayo Askofu Laiser
alimpa siku aliyomtembelea hospitalini kwake, Februari 3, ni kuwa
asimamie ukweli daima kwani ukweli utamlinda. Mbowe alitoa wito
katika msiba huo viongozi wote waliofika kuendelea kuimarisha
unyenyekevu na mshikamano ambao wameonyesha katika dhana nzima ya
kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.
Alisema vi vyema ijulikane kuwa maisha na vyeo
ni vya kupita na hakuna chama ambacho kitaongoza milele siyo CCM wala
Chadema, hivyo hakuna sababu ya Watanzania kugombana. “Hivi sasa tupo
katika taifa lenye hofu, tunaomba viongozi wa dini watuongoze sisi
wanasiasa na watuambie ukweli bila ya kuficha,” alisema Mbowe. Alisema
viongozi wa dini wanahubiri amani lakini pia ijulikane kuwa amani ni
tunda la haki.
|
0 Comments