DAKAR, Senegal
WAZIRI wa Haki nchini Senegal,  Aminiata Toure, amependekeza makahaba wote nchini humo wapewe vitambulisho maalum.
Matamshi yake yalitolewa huku nchi hiyo ikijiandaa kwa kongamano muhimu wiki ijayo kuhusu sheria za ukahaba.
Toure alisisitiza kuwa kadi hizo zipewe tu wanadada waliozidi miaka 18, na watakaokiuka hilo wakamatwe na kushtakiwa.
Vitambulisho vimekuwa vikitolewa bila malipo kwa makahaba tangu miaka 20 iliyopita lakini kwa machangudoa wanaoendesha biashara yao mjini Dakar na mitaa viungani.
Waliopewa kadi hizo walichunguzwa vikali na walihitaji kila mwezi kupita kipimo cha HIV/Ukimwi ama maambukizi mengine ya zinaa.
Waliokuwa wanaishi  bila maradhi walitakiwa kutoa damu iliyowekwa katika hifadhi na kupewa hospitali.
Waliopatikana na maambukizi madogo walitibiwa na kuruhusiwa kwenda, na waliopatikana kuwa na vijidudu vya maambukizi walitengwa kando.
Juhudi hizo za tangu miaka ya mapema ya themanini kuhamasisha umma kuhusu janga la ukimwi, zinaaminika kupelekea Senegal kuwa miongoni mwa mataifa yaliyo na kiwango cha chini sana cha maambukizi ya HIV barani Afrika.
Kikosi maalum
Lakini kongamano hilo la Jumatano linanuia kung’oa watoto katika biashara hiyo na kuweka msingi wa sheria zenye uhalisi, kali na thabiti na mikakati ya kudhibiti ukahaba nchini Senegal.
Waziri huyo  pia alipendekeza kikosi maalum kilichoundwa kuwafuatilia mahakaba kipewe vifaa vya kutosha na vizuri vya kuwawezesha kutekeleza jukumu hilo.
“Ili kudhibiti vyema ukahaba nchini Senegal, twahitaji ushirikiano wa wadau kadha kama viongozi wa kidini na muhimu zaidi wadau katika sekta ya utalii na burudani.”