Dar es Salaam. 
  Wakati Kiongozi wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila akitiwa mbaroni kwa tuhuma za uchochezi wa kidini, viongozi wa Jumuiya  ya Kiislamu Tanzania wametoa tamko na kusema kuwa baadhi ya kauli za viongozi wa Serikali na viongozi wa dini zina mwelekeo wa kukuza mfarakano wa kidini kuliko kuleta maelewano.
Wiki iliyopita Mchungaji Mtikila alikamatwa mkoani Rukwa akituhumiwa kuwahamasisha Wakristo wawavamie Waislamu.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema Mchungaji Mtikila alichochea uhasama kwa kuwaeleza viongozi wa Kikristo kuwa, wamekuwa wakionewa na Waislamu kutokana na matukio yanayoendelea kutokea hapa nchi.
Katika tamko lao, viongozi wa  Kiislamu walisema kuwa mara nyingi kauli  za viongozi wa dini na Serikali hazina nia njema bali zimekuwa za kibaguzi au za kiupendeleo.
“ Imekuwa ni kawaida kila anaposhambuliwa au kuuawa Padri baadhi ya viongozi wa Serikali, na wale wa Kikristo, vyombo vya habari, baadhi ya asasi na taasisi za kiraia wamekuwa wakiwanyooshea vidole na kuelekeza lawama zao kwa jamii ya Waislamu,” lilisema tamko hilo.
Katika tamko hilo Jumuiya ya Waislamu ilieleza kuwa Waislamu wamekuwa wakinyooshewa vidole kutokana na matukio hayo pasipo kuwa na ushahidi.
Iliongeza kuwa wamekuwa wakishutumiwa kuhusika katika matukio kabla hata ya  uchunguzi wa vyombo vya usalama na polisi kufanyika.
Tamko hilo lilisema kuwa serikali kupitia waziri wa mambo ya ndani ilitoa kauli kuwa mauaji ya padri huyo ni matokeo ya kazi za ugaidi.
Tamko hilo lilisisitiza kuwa linaungana na wapenda amani wote kulaani mauaji, manyanyaso  na udhalilishaji wa aina yoyote unaowalenga viongozi wa dini.
Jumuiya hiyo imewataka viongozi wa dini na Serikali kuhakikisha wanahimiza  amani na mshikamano badala ya kuwa vyanzo vya kuchochea vurugu.
Wamesema hawatafumbia macho tabia ya kuendelea kunyoshewa vidole Waislamu kila linapotokea tukio la uvunjifu wa amani nchini na wamewataka Watazania wote kwa umoja wao kusimamia ushirikiano na kuiimba amani ili kulinusuru taifa na aina yoyote ya vurugu.