Dar es Salaam. Bunge limeingia katika mzozo mwingine na Chadema baada ya kudaiwa kutoa ripoti polisi likitaka wabunge 28 wa upinzani waitwe ili wahojiwe katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na fujo zilizotokea bungeni Februari, mwaka huu.

Hata hivyo, chama hicho kikuu cha upinzani kupitia kwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, kimepinga hatua hiyo kikisema kamati hiyo haipo kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 113(7) kwa kuwa imemaliza muda wake tangu Februari 8, mwaka huu na Spika hajaunda nyingine.

Hata hivyo, madai hayo ya Lissu yamepingwa vikali na Naibu Spika, Job Ndugai ambaye amesema kamati hiyo pamoja na nyingine mbili za Uongozi na ile ya Kanuni zinatambulika mpaka zitakapoundwa nyingine... “Hizo tatu ni ‘ongoing’ (zinaendelea) zisipokuwapo, basi Bunge hakuna.”

Mvutano huo ni wa pili katika siku za karibuni baada ya ule uliotokea katika Kikao cha Bunge la Februari baada ya Wabunge wa Chadema kuzua tafrani zilizosababisha kukatishwa kwa kikao kimoja cha Bunge hilo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Lissu alisema yeye na wabunge wenzake wapatao 28 watafika mbele ya kamati hiyo lakini wamekubaliana kuwa hawako tayari kuhojiwa nayo.
Mbali ya Lissu, jana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara mjini Musoma alisema wabunge wa chama chake hawatakwenda kuhojiwa na kamati hiyo.

Lissu alisema njia iliyotumika kuwaita mbele ya kamati hiyo kwa kupitia polisi ni kinyume na utaratibu.
“Utaratibu uliotumika ni haramu kwa kuwa polisi ndiyo wametumika kutujulisha kwamba tunatakiwa tufike mbele ya kamati hiyo, kutumiwa ujumbe wa polisi si sawa kwani utaratibu wa Bunge unajulikana,” Lissu alisema na kuongeza:

“Kamati iliposema bungeni kuwa mimi na wenzangu watatu ni vinara wa fujo ilituhukumu tayari, hivyo kisheria wale wengine waliobaki walikuwa hawana makosa kwa mujibu wa sheria zetu.”

Ilidaiwa kwamba Ofisi ya Bunge iliiandikia Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kutaka kuwaelekeza makamanda wake kufikisha taarifa hizo.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema hakuwa na taarifa hizo na kuahidi kufuatilia.

Alipoulizwa kuhusu wabunge hao kuitwa kwa kutumia polisi, Ndugai alisema hakuwa na taarifa hiyo na kuelezea wasiwasi kwamba suala hilo limefikia hatua hiyo.
“Sidhani kama imefikia huko (kutumia polisi kuwaita wabunge), kwani kamati ina utaratibu wake wa kumwita mtu yeyote hata asipokuwa mbunge, kwa kweli sijui na sifikirii kama watakuwa wamefikia huko,”alisema Ndugai.

Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kumpigia simu Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kumpa wito wa kufika mbele ya kamati hiyo ya Bunge na pia alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karatu (OCD), kuwapa taarifa Mbunge wa Karatu, Israel Natse na Mbunge wa Viti Maalumu Cecilia Paresso.