Madini ya Tanzanite

Burundi
Nchi hiyo inaongoza kwa watu wake kuwa maskini kwa asilimia 81.32

Tanzania
Inashika nafasi ya pili kwa Watanzania kuwa maskini kwa asilimia 67.87

Rwanda
Rwanda ni ya tatu kwa watu wake kuwa katika hali mbaya kiuchumi  kwa asilimia 63.17

Kenya
Nchi hiyo ya nne kwa watu wake kuwa maskini kwa asilimia 43.37

Uganda
Ni ya tano kwa Waganda kuwa maskini kwa asilimia 38.01
.

Nchi ya Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa kuwa na watu maskini kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiongozwa na Burundi.

Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwaka huu, umebaini kwamba katika nchi za Afrika Mashariki, Uganda inaongoza kwa kutokuwa na watu maskini.

Utafiti huo ulibaini Tanzania ina asilimia 67.87 ikifuatiwa na Burundi ambao wana asilimia 81.32. Ukiacha Tanzania nchi inayofuatia ni  Rwanda ambayo utafiti huo ulibaini kuwa ilikuwa na asilimia  63.17, huku  watu wa Kenya wakiwa na alama za umaskini kwa asilimia 43.37,  Uganda 38.01.

Kwa mujibu wa ripoti ya Global Monitoring ya mwaka 2013, matokeo ya utafiti huo yaliangalia idadi ya watu wanaoishi kwa Dola 1.25 sawa na Sh2,000 kwa siku.Kwa utafiti huu, Tanzania na Burundi zinakuwa nchi zenye idadi kubwa ya watu maskini katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi za chini ya jangwa la Sahara zinajikongoja katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Mwaka 1990 nchi za chini ya Jangwa la Sahara na Asia Mashariki zote zilikuwa na asilimia 55 wakati zilipoanza safari ya kuelekea maendeleo ya milenia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,  mwaka 2010 Asia Mashariki ilifanya jitihada kubwa za kupunguza umaskini hadi kufikia asilimia 12 wakati nchi za chini ya Jangwa la Sahara zilikuwa zina asilimia 48 ya umaskini.
Barani Afrika ukuaji wa miji umeongeza kutoka asilimia 30 mwaka 1980 hadi asilimia 50 mwaka 2011.

“Ukuaji wa miji unasaidia watu kuondokana na umasikini na kuelekea katika malengo ya Milenia, lakini kama hautasimamiwa vizuri unaweza kusababisha ukuaji holela wa miji, uchafuzi wa mazingira na ongezeko la uhalifu,” inasema ripoti hiyo.

Zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa zinazozalishwa ulimwenguni zinazalishwa mijini, na kusababisha ukuaji wa miji na kupunguza umaskini. Nchi nyingi za Asia Mashariki na Marekani zimefanikiwa sana kupunguza umaskini kwa kupiti njia hii.

“Kinyume chake, Asia Kusini na nchi za chini ya Jangwa la Sahara zina idadi kubwa ya watu maskini na zinaendelea kujikongoja kuelekea katika maendeleo ya Milenia.” inabainisha sehemu ya ripoti hiyo ya WB.

Wachumi Tanzania
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Tanzania, Dk Honest Ngowi anasema kimsingi umaskini ulioanishwa na ripoti hiyo ni umaskini wa kipato na anasema licha ya kuwa tuna raslimali nyingi kama madini, utalii na nyingine, lakini hoja inayokuja ni je zinatumiwa vipi?“Ni sawa madini yanachimbwa, lakini wawekezaji ndiyo wengi, lakini sekta hii ya madini haina mwingiliano wa moja kwa moja na watu, na kama watu wa kawaida hawahusiki moja kwa moja inakuwa vigumu kuinuka kimapato,” anasema mhadhiri huyo.
Mtaalamu huyo wa uchumi anabainisha kwamba ili mtu awe na kipato ni lazima afanye kazi.