Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupigia kura
azimio linalopendekeza kuundwa kwa kikosi cha kulinda amani nchini Mali.
Kikosi hicho chenye wanajeshi 12,600 kinajumuisha takriban wanajeshi 6,000
kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika ambazo tayari zina wanajeshi wao nchini
humo.
Azimio hilo limependekezwa na Ufaransa ambayo iliingilia kati mzozo wa Mali
mnamo mwezi Januari ili kupambana na wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini mwa nchi
hiyo.
Kikosi hicho kinatarajiwa kwenda Mali mwanzoni mwa mwezi Julai kabla ya
uchaguzi mkuu.
Hata hivyo duru zinasema kuwa azimio hilo limezua mjadala mkali.
Makundi ya kiisilamu yaliweza kutumia pengo la usalama lililotokea baada ya
mapinduzi ya kijeshi mwaka jana na kuanza kushinikiza watu kufuata sheria za
kiisilamu.
Miji iliyo Kaskazini mwa nchi, imeweza kudhibitiwa na jeshi la Ufaransa
lakini baadhi ya wapiganaji wangali katika maficho yao.
Ufaransa ilianza kuondoa baadhi ya wanajeshi wake 4,000 mapema mwezi huu
kutoka nchini humo, lakini imekuwa ikishinikiza Umoja wa Mataifa kupeleka
wanajeshi wake.
Aidha wanajeshi wa Chad, wanasemekana kuwa wenye uzoefu mkubwa zaidi katika
kupambana na wapiganaji jangwani, lakini nchi hiyo pia imeanza kuondoa wanajeshi
wake kutoka Mali.
Sababu ya kikosi cha Umoja wa mataifa ni kulinda amani na kitakuwa na
wanajeshi 11,200, pamoja na polisi 1,440.
Lengo lake kuu litakuwa kuweka uthibiti katika baadhi ya sehemu za Kaskazini
mwa Mali ili kumaliza vitisho kutoka kwa wapiganaji wa kiisilamu.
Hata hivyo rasimu ya azimio hilo haisemi ikiwa wanajeshi hao wataweza
kupigana na wapiganaji wa kiisilamu wenye uhusiano na kundi la al-Qaeda, lakini
wanajeshi 1,000 wa Ufaransa,wataweza kusalia Mali. |
0 Comments