Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametoa siku 30 kubomolewa kwa jengo lingine lenye ghorofa 16 lililopo mtaa wa Indira Gandhi, jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kuwapo na ukiukwaji wa sheria ya mipango miji.
Profesa Tibaijuka aliyasema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili ilipotembelea eneo jengo la ghorofa 16 lililoporomoka wiki iliyopita na kusababishia vifo vya watu 36.
Mbali na adhabu hiyo, mmiliki wa jengo akikaidi agizo hilo atalipishwa faini ya asilimia mbili ya gharama ya maelezo yasiyokuwa na kibali kwa kila siku hadi atakapotelekeza agizo hilo.
Profesa Tibaijuka alisema imebainika kuwa jengo lililoko mkabala na eneo hilo kwenye kiwanja namba 1662/75 chenye mita za mraba 150 limejengwa kwa viwango visivyokidhi kanuni za upangaji miji vilivyoainishwa kwenye mpango wa uendelezaji upya wa eneo la kati la jiji la Dar es Salaam wa mwaka 2000.
“Idara yangu imetafiti suala hili na kugundua kuwa ujenzi huo haujapata idhini ya nyongeza ya sakafu sita kwenye kiwanja kilichotajwa hivyo ujenzi wa sakafu 16 umekiuka mpango huo na taratibu za kisheria,” alisema Profesa Tibaijuka Waziri Tibaijuka alisema kwa kuzingatia kifungu cha 54 cha sheria ya mipango miji ya mwaka 2007, anafuta idhini ya uendelezaji (Planning consent) wa kiwanja hicho kwa sababu ujenzi huo umekiuka masharti ya uendelezaji.
Alisema kulingana na sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, kifungu cha 44 na 45 na pia kanuni za ardhi za 2001 inaelekeza mhusika aliyekiuka masharti ya uendelezaji anapaswa kupewa ilani ya kubomoa na akiendelea kuikaidi amri analipa faini ya asilimia mbili.
Profesa Tibaijuka pia amewataka viongozi wa Manispaa ya Ilala kufanya ukaguzi wa majengo yote yanayojengwa ili kujiridhisha na ubora pamoja na uzingatiaji wa kanuni na taratibu za ujenzi na mipango miji.
“Kuna baadhi ya majengo yamepewa kibali na yanajulikana kama BoT halina shidam, na yale ambayo yatabainika kuzidishwa bila kibali maalumu nayo yajiandae kubomolewa lazima tufuate sheria kwa sasa watu watagonga mwamba wamezoea kukiuka sheria,” alisema Tibaijuka.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kujiridhisha na kuepuka madhara yasiyo ya msingi kutokea kwa umma.
Alisema kuna baadhi ya wamiliki wa majengo hawapeleki maombi ya nyongeza za sakafu wakati ujenzi unaendelea au umeshakamilika na kwamba jambo hilo haliwezi kukubalika kwani inajenga hisia ya udanganyifu.Profesa Tibaijuka alisema wakati wakisubiri uamuzi wa mahakama na matokeo ya uchunguzi wa kamati mbalimbali zilizoundwa pamoja na vyombo husika kuchunguza sababu za kuporomoka kwa jengo hilo, ametoa onyo kwa Halmashauri ya Ilala kutokukiuka taratibu za upangaji na uendelezi wa miji.
Aidha alisema endapo halmashauri hiyo ya Ilala itaendelea kushindwa kusimamia sheria ya mipango miji na kusababisha maafa itanyang’anywa Mamlaka ya upangaji chini ya kifungu namba 7(4) cha sheria ya mipango miji ya namba nane ya 2007.
Pia Waziri Tibaijuka alishauri kuwapo kitengo kitakachosimamia ujenzi.
Profesa Tibaijuka alisema kuna taarifa zinazodai kuwa mmiliki wa jengo lililoanguka alikuwa na miradi mitano ya ujenzi ambapo Tibaijuka alimtaka Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba (NHC) Nehemiah Mchechu kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo.
Mchechu alikiri mmiliki huyo kuwa na miradi mitano ya majengo na kati ya hiyo mitatu watu wanaendelea kuishi.
Mchechu alisema tayari wameshawasiliana na bodi ya wahandisi kwa ajili ya kuchunguza miradi yake ili kubaini kama majengo yapo katika kiwango kinachotakiwa ili yasije kusababisha madhara mengine.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk. Terezya Huvisa alisema kuwa mwekezaji yeyote anayetakiwa kufanya ujezi wowote ambao ni zaidi ya ghorofa tano ni lazima aombe kibali cha tathimini ya mazingira katika ofisi yake.
Alisema wengi wao wamekuwa hawataki kuifuata sheria hiyo kabla ya mtu kuanza mradi ili aweze kupatiwa ushauri wa kimazingira.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, James Lembeli alimshukuru Waziri Tibaijuka kwa maamuzi mazito aliyoyafanya na kumtaka asimamie utekelezaji wa ubomoaji wa jengo hilo.
Naye Rais wa Jumuiya ya Khoja Shia Thnacesheria, Azim Deuji, alimuomba waziri Tibaijuka kuhakikisha watu wa msikitini ama makanisa kupatiwa elimu juu ya miradi ya ujenzi wa maghorofa ili waweze kuitoa kwa waumini wao.
|
0 Comments