Mjane wa marehemu Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere
Mjane wa marehemu Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amewataka wanawake nchini kuishi kwa kuheshimiana, kushirikiana na kusaidiana kwa lengo la kupambana na ukatili wa kijinsia.

Mama Maria aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akifungua mkutano wa viongozi wanawake katika sekta mabalimbali na siasa uliofanyika mkoani Mara.

Alisema kuwa ili ukatili wa kijinsia uweze kuisha au kutokomea ni lazima wanawake wenyewe wajitambue katika nafasi aliyonayo kwa kuhakikisha elimu ya kuzuia ukatili wa kijinsia inatolewa na kila mmoja katika eneo alilopo.

“Sisi wanawake hatupendani, lakini kama tukianza kupendana sisi kwa sisi hakika ukatili wa kijinsia utaisha, kwa sababu chanzo cha ukatili wa kijinsia ni mfumo dume na mfumo dume tunaukaribisha sisi wenyewe,” alisema Mama Maria.

Alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaonekana kushamiri sana mkoa wa Mara kwa sababu wanawake walio wengi mkoani hapa hususani walio vijijini wanaendekeza mfumo dume na pia huendekeza imani za mila potofu.


Mama maria aliongeza kuwa watoto wa kike mkoani hapa huishi kwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia lakini wao hawalitambui hilo kufuatia mazingira waliyokulia ya kuona ni jinsi gani mama zao wanavyofanyiwa na baba zao.

“Watoto wa kiume hapa mkoani kwetu ni wakatili na tena huwafanyia watoto wa kike na hata mama zao kwa sababu wamekuwa wakiona baba akifanya ukatili kwa mke wake, mama na hata dada zao, hivyo nao huona ndivyo wanavyotakiwa kufanya,” alisema Mama Maria.

Aidha, aliwataka wanawake walio na nyadhifa mbalimbali kuhakikisha wanasaidiana na mashirika yanayopambana na ukatili wa kijinsia ili kutoa elimu kwa jamii.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Vijijini (TARWOC), Lediana Mng’ong’o, alisema kuwa nia na madhumuni ya kuandaa mkutano huo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu maendeleo kwa wanawake na wasichana na pia kuhimiza elimu kwa watoto wa kike.

Mng’ong’o alisema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa katika bara la Afrika, Tanzania ina asilimia 44 za ukatili wa kijinsia huku kwa hapa nchini mkoa wa Mara unaongoza kuwa na ukatili wa kijinsia kwa asilimia 72 ukifuatiwa na mkoa wa Dodoma kwa asilimia 71.




 

CHANZO: NIPASHE