Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewatuliza Watanzania kuhusu kupanda kwa nauli akisema ameyapokea malalamiko  yao na atayafanyia kazi. Kwa kuanzia ameagiza nauli za treni jijini Dar es Salaam zisipande bali ziendelee kutozwa za zamani  mpaka taarifa zaidi itakapotolewa.
Mwakyembe alitoa kauli hiyo alipozungumza kwenye Bonanza la Vyombo vya Habari lililofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ni kweli Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra|) ilitangaza nauli mpya, lakini kwa kilio cha Watanzania ataangalia sababu za kupandisha huku akishirikiana na wasafirishaji kujua ukweli. Kuhusu tuhuma za Chadema dhidi yake kwamba amefanya ufisadi kuipatia Mamlaka ya Bandari(TPA) kiwanja cha Kampuni ya Jitegemee inayomilikiwa na CCM ili CCM inufaike,  alisema hizo ni njama za mafisadi waliokuwa wakikitaka kiwanja hicho kutaka kuichafua Serikali na yeye.
“Nawahakikishia kwamba  TPA iliomba kama kampuni zingine na mimi nataka TPA ipate eneo la kuhamishia mizigo na kamwe sintampenda mafisadi wapate kiwanja hicho’’ alisema.Waziri Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela aliwasihi Chadema na mafisadi wanaotaka kuvitumia vyama vya siasa waendelee kumchafua na kwamba yeye hatachoka kwa vile malengo ni kuwatumikia Watanzania.

Pia aliwashtua waandishi alipotamka waziwazi kwamba yeye hana ndoto za kugombea urais mwaka 2015, lakini anachapa kazi ili awe Waziri Bora wa Uchukuzi.

Mwakyembe ambaye ni mwanasheria na mwandishi wa habari alitumia muda huo kuwasihi waandishi nchini kuacha kupenda mishiko kwa nia ya kupotosha ukweli.

Hata hivyo aliwapongeza  akisema ni jambo la busara kukutana na kutathimini utendaji kazi.
Awali Katibu wa Chama cha Waandishi wa habari za Michezo (Taswa0 ambacho kiliratibu hafla hiyo, Amir Mhando alisema walimwalika Dk Mwakyembe baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wake.