Anasema mara nyingi wamekuwa wakiwalaza watoto sebuleni bila kujali jinsia zao, kwamba wakati mwingine iliwazazi wanapohitaji kukutana faragha huwalazimu kwenda kulala katika nyumba za wageni.
“Huwezi kufanya faragha na mkeo huku watoto wakiwa wamelala sebuleni halafu wa jinsia moja hivyo kwa sisi wengine tunaamua kuingia gharama nyingine ya kwenda kulala katika nyumba za wageni ili kuepuka kuwaharibu watoto kisaikolojia,” anasema.
Askari mwingine kwa sharti la kutotajwa jina anasema mazingira ya nyumba hizo ni machafu na kuna msongamano mkubwa wa watu hasa katika huduma ya choo kwani hutumiwa na watu wengi.
“Ukitaka kuona adha ya choo ni muda wa asubuhi ambapo kila mmoja anahitaji huduma ya bafu kwa ajili ya kuoga na kuwahi kazini, inakuwa kama sinema vile hivyo mazingira ya nyumba zetu bado hayafai…,” anasema.
Kwa upande wake Koplo Atupele anasema kuwa kwa wale ambao ndiyo wanaanza kazi hupangiwa kulala kwenye bwalo ambapo hutandika magodoro chini, hulala eneo hilo mpaka watakapopata nafasi katika nyumba za serikali.
“Ndiyo maana utakuta askari wengine wanaamua kwenda kuishi uraiani ili kukwepa adha ambayo wanaipata kwenye kota,” anasema.
Anasema maisha halisi ya polisi kwa kiasi fulani yanachangia kujiingiza katika vitendo vya kupokea rushwa na kukiuka maadili.
Mtwara
Maisha duni kwa askari polisi wa vyeo vya chini nchini yanaelezwa na baadhi ya polisi mkoani Mtwara kuwa ni chanzo cha wao kujiingiza katika vitendo vya uhalifu na unyanyasaji kwa wananchi.
“Kwa ujumla mazingira ni duni, tunakwenda lindoni tukiwa hakuna sehemu maalum kwa ajili ya lindo, mvua yetu, jua letu, ukirudi ofisini mabosi nao wanakunyanyasa…, ili uishi vizuri kwa sisi askari wadogo ni lazima ‘uji-attach’ na bosi ambaye akikupangia kazi yenye maslahi lazima umuachie kitu kidogo (fedha)” anasema mmoja wa polisi hao.
0 Comments