Wanawake kutoka Umoja wa Wanawake Wakristo (YWCA), wakiandamana Dar es Salaam juzi, kuadhimisha siku ya umoja huo kimataifa, suala la ukatili dhidi yawanawake ni ajenda iliyokuwa imetawala. Picha na Joseph Zablon


Morogoro. Polisi mkoani Morogoro wanamshikilia mkazi wa mjini hapa kwa tuhuma za kumbaka na kumsababishia maumivu makali mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka minane mwanafunzi wa darasa la kwanza.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, John Laswai alisema kuwa tarehe na muda usiofahamika mwanaume huyo kwa muda mrefu alikuwa akimwingilia kimwili mtoto wake huyo anayesoma katika shule ya msingi.

Laswai alisema kuwa mwanaume huyo siku ya tukio alimwingilia mtoto wake, lakini kabla ya kufanya kitendo hicho alimtuma mtoto wake wa kiume ambaye ni bubu mwenye umri wa miaka 13 dukani mtoto huyo aliporudi alikuta baba yake akitaka kumfanyia unyama huo mdogo wake ndipo alimsadia na wakati wakitaka kukimbia baba alimshika mtoto wa kike na kumfungia ndani.
Kaimu kamanda huyo alisema kuwa baada ya mtoto wa kiume kuona mdogo wake kafungiwa ndipo alipotoa taarifa kwa majirani na kwenda polisi kutoa taarifa,baada ya polisi kufika walimkuta baba huyo akimbaka mwanaye huyo huku akiwa amempiga na kumchoma moto sehemu za usoni.

Alisema kuwa baba huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika na kwamba mtoto kwa sasa yuko katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Mtoto huyo akizungumza kwa taabu namna ilivyokuwa alisema kuwa baba yake amekuwa akimfanyika kitendo hicho mara kwa mara na anapokataa huwa anampiga na kumtishia kumuua na aliongeza kuwa yeye na kaka yake wamekuwa wakiishi katika hali ya mateso kutoka kwa baba yao na kwamba mama yao aliachana na baba huyo na yuko mkoani Singida

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Grace Massawe akizungumza hospitalini hapo alikiri kumpokea mtoto huyo huku akiwa katika maumivu na majeraha sehemu za usoni.