Wachezaji wa timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam wakishangilia kwa staili yake .

Msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2012-13, utamalizika hapo Mei 18, na tayari Yanga ameshatangazwa kuwa bingwa akiwa na mechi mbili mkononi.
Kwanza kabisa nizipongeze timu zote 14 zilizoshiriki ligi hiyo kwa kuonyesha kiwango kizuri cha uchezaji pamoja na kuwepo kwa matatizo ya hapa na pale.
Nasema hivyo kwa sababu hata timu kama Toto Africans, Polisi Morogoro na African Lyon ambazo zimeshuka daraja zilionyesha kiwango cha kuridhisha ingawa mwishowe ilikuwa ni lazima timu 3 ziporomoke daraja ili zizipishe nyingine tatu ziweze kupanda.
Pongezi zangu pia nazielekeza kwa klabu za Yanga na Azam kwa kufanikiwa kutwaa nafasi mbili muhimu za juu katika ligi hiyo.
Kama ilivyo kawaida kizuri nacho huwa hakikosi kasoro, pamoja na yote hayo kuna baadhi ya kasoro zilizojitokeza katika msimu wa ligi uliomalizika ambao kimsingi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)linatakiwa kurekebisha ili zisijitokeze katika msimu ujao na kuathiri mwenendo wa ligi.

Tulishuhudia TFF ikibadili mara kwa mara ratiba ya ligi hatua ambayo ilipelekea kuahirishwa kwa baadhi ya mechi kwa kuzisogeza mbele na wakati mwingine kurudisha nyuma.

Mabadiliko haya yalisababishwa hasa na mwingiliano wa kalenda ya TFF na ile ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na yalitokea mara nyingi wakati wa shughuli za kiserikali.
Ni dhahiri kwa kitendo hiki cha TFF kubadili ratiba mara kwa mara kilisababisha bajeti za timu kuparaganyika na hivyo kuziongezea mzigo wa gharama katika kujiendesha.

Hakuna ubishi katika hili, kwa vyovyote vile timu inapopewa ratiba inayoonyesha tarehe fulani itacheza na timu fulani alafu ghafla inapewa taarifa nyingine ya kuahirishwa kwa kusogeza mechi mbele maana yake ni kwamba italazimika kuongeza bajeti yake iliyokuwa imetenga la sivyo itashindwa kumudu gharama.

Pia, athari nyingine zinazoweza kuzipata timu kutokana na mabadiliko ya ratiba ya mara kwa mara ni kuharibika kwa programu za makocha pamoja na saikolojia ya wachezaji.

Tunafahamu kwamba makocha nao wana programu zao kulingana na ratiba na mechi zinazoihusu timu yake, lakini wachezaji nao huathirika kama ilivyo askari wanaojiandaa kwa vita wanakuwa na maandalizi yao ya kimwili na kiakili.

Kuna haja ya TFF kuliangalia hili kwa umakini zaidi kwa kupanga ratiba ya ligi itakayoendana na kalenda ya Fifa ili kila upande usiathirike kwa namna yoyote ile.