Baadhi ya washiriki wa Tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere.
Suala la Afrika kujitawala na kujitegemea katika nyanja zote limekuwa mjadala wa muda mrefu kutoka kwa Waafrika wenyewe.
Kwa muda mrefu Bara la Afrika limeonekana kuwa nyuma katika maendeleo ya uchumi, jamii na siasa.
Baadhi ya wapelelezi wa wakoloni katika karne ya 18 walilitaja bara hilo kama la giza kutokana na hali ya kudorora kimaendeleo kulinganisha Ulaya walikotoka. Licha ya kuja kutawala kwa takriban karne moja, wakoloni kutoka Ulaya wameendelea kuzitawala nchi za Afrika kwa ukoloni mambo leo. Suala la Afrika kujitawala na kujitegemea katika nyanja zote limekuwa mjadala wa muda mrefu kutoka kwa Waafrika wenyewe.
Mjadala huo umeibuka pia katika tamasha la tano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, ililofanyika hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam likiwa limebeba ujumbe wa “Maendeleo ni mapambano ya Ukombozi,” suala la Afrika kujitawala limetawala.
Akitathmini falsafa ya maendeleo ya Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Manuh Takyiwaa kutoka chuo Kikuu cha Ghana, Legon anasema pamoja na Afrika kuwa na maliasili nyingi, bado wapo viongozi ambao wanazigombania kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi huku wakiwaacha wananchi mikono mitupu.
Anahoji falsala ya kujitegemea na kama rasilimali yaani watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora zinatumika ipasavyo.“Waafrika bado wanagombania maliasili zao, nyingine zikichukuliwa na kusafirishwa nje kwenda kuyanufaisha mataifa ya mbali. Hata kitendo cha kuikumbatia China kinaonyesha kuwa hatuja jifunza chochote,” anasema Takyiwaa.
Naye Profesa Penina Mlama kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anatoa mfano wa utegemezi wa Watanzania kiasi cha kuwataka hata wahisani wachangie ujenzi wa vyoo vya shule. “Shule nyingi vijijini hazina vyoo… Nimekutana wa wakuu wa shule wanaosema tunasubiri wahisani watusaidie. Nini kinachotufanya tuwasifu na kuwatetemekea baadhi ya viongozi ambao tunajua kabisa wanalimaliza taifa letu?”
Profesa Mlama kwa upande mwingine anasema hali imekuwa mbaya zaidi hata kwa baadhi ya wasomi, ambao wamekuwa wakifundisha njia sahihi ya kufuatwa huku wakiwanyooshea vidole wengine, lakini hivi sasa wameanza kwenda kando na kuanza kuyatenda yale waliyokuwa wakiyapinga.
“Tunapozungumzia mustakabali ukombozi wa kimaendekeo ni lazima tupate suluhisho la hii nguvu inayoleta haya yote. Watu wapo, lakini ni wa aina gani?”
Kwa upande wake Profesa Monica Lima e Souza kutoka Chuo Kikuu cha Federal cha Rio Dejaneiro, anatoa uzoefu wa Brazil ambayo imepiga hatua katika kujikomboa kwa kuanzisha mtalaa wa masomo katika vyuo vikuu unaolenga kujikomboa kimaendeleo kupitia fikra za Kiafrika.
“Tusiwe na mwelekeo mmoja katika kufikia malengo yetu. Tunazungumzia bara nzima, turuhusu mawazo tofauti kutoka kila kona ili tuwe na nguvu ya kufika kule twendako,” anasema Souza.
Brazil ambayo nusu ya watu wake wana asili ya Afrika, pamoja na kuwa katika orodha ya nchi zinazoibuikia katika uchumi, bado inakabiliwa na matatizo lukuki. “Wanasema Brazil ipo katika kundi la nchi zinazokuwa kiuchumi. Sawa, lakini watu wengi wana hali mbaya kiuchumi,” anasema Souza.
|
0 Comments