Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma, Venance Mwamoto(kushoto) wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge Dodoma jana wakifuatilia kikao cha Bunge. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Dar es Salaam.
 Wadau mbalimbali wameuponda uongozi wa Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu kutokana na tabia ya baadhi ya Mawaziri na Wabunge kutohudhuria vikao vya Bunge.

Maoni ya wadau hao yamekuja siku moja baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kuomba mwongozo kwa Naibu Spika Job Ndugai ili aone haja ya kusimamisha mjadala wa Wizara ya Kilimo,Chakula na Ushirika kutokana na idadi ndogo ya mawaziri waliokuwapo Bungeni.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ali amesema kinachotokea ni udhaifu wa kiuongozi kwani mawaziri wote wanatakiwa kuwajibika kwa Waziri Mkuu na wabunge wanatakiwa kutokuwapo nje ya Bunge bila ya kupata ruhusa kwa Spika.
Bashiru amesema pia hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na udhaifu wa sheria.
“Kwa upande mwingine hali hii inasababishwa na udhaifu wa sheria na inatakiwa kuwe na sheria inayompa mamlaka mpiga kura uwezo wa kumfuta kazi mbunge na siyo kusubiri baada ya miaka mitano,” alisema Bashiru.


“Ndiyo sababu watu wanataka mawaziri wasiwe wabunge” aliongeza.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi(CUF), Julius Mtatiro alisema anashangazwa kuona hata wabunge makini hawapo bungeni wakati vikao vikiendelea.“Hili ni tatizo unakuta wakati Bunge linaendelea wabunge wengine wanafanya mikutano na wanachi wao, muda wa Bunge uwe wa Bunge na muda wa mikutano na wanachi nao uwe muda wa mikutano” alisema.


“Hii inatokea kwa sababu Serikali ni dhaifu na hakuna umakini, tuangalie wenzetu Kenya hata katika Bunge lao lililopita huwezi kukuta mambo kama hayo,” alisema.
Mtatiro alisema wabunge wanalipwa mshahara wa Sh12 milioni kwa mwezi lakini hawafanyi kile wanachotakiwa kufanya.


Mwanasiasa huyo kijana alisema inatakiwa kuwe na sheria ambazo zinamdhibiti kiongozi wa umma asipokuwa kwenye eneo lake la kazi“Nchi hii haiko serious(makini) na hili ni tatizo lipo kila mahali, ukienda hospitali utakuta madaktari utaambiwa daktari ameenda kula wakati mgonjwa yuko hoi, sasa ni ugonjwa gani unaoweza kusubiri hali hiyo?” Alihoji Naibu Katibu Mkuu huyo.


Naye Katibu Mkuu wa chama cha NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza alisema kutokuhudhuria vikao kwa mawaziri na wabunge huenda kukawa kunasababishwa na shughuli nyingine za kibunge.“Tusilaumu sana tuangalie hawakuwapo kwa sababu gani,tatizo tunachukulia mambo kishabiki,labda walikuwa katika vikao vingine,”alisema Ruhuza.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia hilo wamesema kukosekana kwa uzalendo kunachangia mambo hayo.


“Lakini pia inabidi zitungwe sheria za kuwabana kama kukatwa mishahara au kuchukuliwa hatua za kinidhamu,”alisema Hans Yusuph mkazi wa Dar es Salaam.
Stephen Abeid alisema haoni ajabu kwani hata tabia ya wabunge kutoa matusi bungeni ni utovu mkubwa wa nidhamu kuliko hata kutokuhudhuria vikao.


Kutokana na idadi ndogo ya mawaziri juzi wakati wa kikao cha mjadala wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Naibu Spika Job Ndugai alisema kuwa mawaziri hao wote wapo Dodoma na walikuwa wakifuatilia kila kitu ndani ya Bunge,ila walikuwa wakiweka mambo sawa ili wasipate shida watakapokuwa wakiwasilisha taarifa zao.