Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam 
                 Cancel
Dar es Salaam.
 Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi amesema hali ya mazingira katika Jiji la Dar es Salaam inatisha na inahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Akizungumza wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Uboreshaji wa Mazingira ya shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Ilala, alisema hatua hiyo inatokana na kuongezeka haraka kwa idadi ya watu pamoja na shuguli za kibinadamu.

Alisema uelewa mdogo wa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira pia umesababisha kuwapo kwa matatizo hasa katika juhudi mbalimbali zinazofanywa za utunzaji wa mazingira.

“Utamaduni wa kuhifadhi na kuendeleza mazingira utiliwe mkazo kwa sababu bila kuwa na mazingira yanayokidhi mahitaji yetu maisha yetu hayawezi kuwa bora,” alisema Mushi.
Alisema tabia za mazingira zimebadilika kutokana na kuongezeka kwa joto suala ambalo ni tatizo duniani kote.

Awali Mratibu wa Maadhimisho hayo, Wema Kajigili, alisema kuwapo kwa maadhimisho hayo kumesaidia kuboreshwa kwa usafi katika maeneo ya shule na kuongezeka kwa uelewa wa wanafunzi ikilinganisha na miaka ya nyuma.

Katika maadhimisho hayo zaidi ya shule 50 za msingi na sekondari zilipewa vyeti, vikombe na vifaa vya kufanyia usafi baada ya kuibuka washindi katika utunzaji wa mazingira.
Mbali na maadhimisho hayo,mikakati mbalimbali ilishauriwa ili kuwezesha  jiji hili kuwa safi na lenye kupendeza, hasa katikati ya Jiji la Dar es Salaam.