Rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza kumalizika kwa muda wa Serikali ya muungano iliyopita, hivyo kufungua njia ya uteuzi wa Baraza Jipya la Mawaziri litakaloongoza Serikali yake.
Hatua ya Kenyatta inamaanisha kumaliza zama za utawalka wa Rais Mwai Kibaki aliyemaliza muda wake, baada ya uchaguzi uliofanyika Machi 4 na kumpa ushindi Kenyatta pamoja na mgombea mwenza wake, William Ruto.
“Kwa mujibu wa Katiba Mpya ya Kenya iliyopitishwa mwkaa 2010, Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mwai Kibaki ilimaliza muda wake usiku wa Aprili 9,” alieleza Kenyatta katika taarifa yake iliyosambazwa na Ikulu ya mjini Nairobi.
Agizo hilo linawahusu wanasiasa waliokuwa katika nafasi za kuteuliwa hasa mawaziri na manaibu wao, ambapo ilieleza kwamba kwa sasa makatibu wakuu wa Wizara ndio watakaoendesha shughuli zote hadi mawaziri wapya watakapotangazwa rasmi.Taarifa hiyo ilitolewa katika siku ya kwanza ya Kenyatta ofisini akiwa mkuu wa nchi, pamoja na msaidizi wake, Ruto, ambapo walikuwa wakipokea taarifa kutoka kwa wakuu wa usalama, maofisa wa Serikali, mwelekeo wa maandalizi ya bajeti na kupitia kwa mara ya mwisho namna ya muundo wa serikali wanayoihitaji.
0 Comments