Dodoma.
 Spika wa Bunge, Anne Makinda jana ni kama aliruhusu mvutano wa wazi baina ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chadema ambao kila upande uliutuhumu upande mwingine kwa kuhusika kwa viendo vya ugaidi.
Licha ya kutozungumzia suala hilo moja kwa moja, lakini msingi wa tuhuma hizo ni kesi iliyofunguliwa mahakamani dhidi ya Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Willifred Lwakatare ambaye anakabiliwa na makosa yanayomtuhumu kwa ugaidi.
Katika mazingira hayo ni dhahiri wabunge waliingilia uhuru wa mahakama kwani kesi husika iko mahakamani na Spika Makinda katika moja ya miongozo yake jana alisema: “Itabidi Kamati ya Kanuni ikutane kwa kuwa mambo yanayozungumzwa yako mahakamani, hivyo ni muhimu mahakama ikaheshimiwa.”
Kifungu cha 114 (1) cha Sheria ya Kanuni za adhabu (Penal Code), kinatoa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela kwa mtu yeyote ambaye kwa namna yoyote anatoa matamshi yenye mwelekeo wa kushawishi uamuzi wa mahakama kwa suala lolote ambalo liko mahakamani likisubiri uamuzi.
Matamshi hayo ni yale yenye mwelekeo wa kupindisha mwenendo wa kesi husika au yenye mwelekeo wa kutaka uamuzi upendelee upande fulani au matamshi yenye lengo la kudhalilisha au kushusha hadhi ya mamlaka ya mtu ambaye kesi yake iko mbele ya mahakama.

Mjadala kuhusu ugaidi ulianza kuchipua juzi wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alipowasilisha maoni ya kambi yake kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu kwa kusema: “Umeibuka uchochezi mpya wa kisiasa wenye ubia kati ya chama tawala na vyombo vya dola na kinachoitwa ugaidi.”

Mbowe alisema kambi yake inashangazwa na uhodari wa Serikali katika kuchukua hatua kwa suala la mtu aliyebambikiwa kesi ya ugaidi kwa ushahidi wa kughushi kuwa yeye ndiye gaidi.

“Kambi yetu inasikitika sana kuona wale wote waliokuwa wakiwasiliana na hao wanaoitwa magaidi ambao pia ni viongozi wa CCM na washirika wao hawajachukuliwa hatua yoyote,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Tunaulaani mkakati huu wenye nia ovu ya kufifisha demokrasia hapa nchini...mpango huu haramu hautafanikiwa ... na hili nalo likiachiwa likakomaa litaliingiza Taifa letu katika hatari nyingine ya machafuko.”
Jana suala hilo lilichukua sura ya kisiasa zaidi pale wabunge wawili; Mwigulu Nchemba wa Iramba Magharibi (CCM) na Tundu Lissu wa Mbunge wa Singida Mashariki walipochangia hotuba hiyo na kuzama katika eneo la ugaidi, hali iliyosababisha mvutano mkali bungeni.

Kauli ya Nchemba

Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara) aliishambulia hotuba ya Mbowe akieleza kuwa hakuna haja ya kuhangaika na suala la ugaidi kwa kuwa Chadema ndiyo wanahusika nalo kwa kupanga kumdhuru mwandishi wa habari.