Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Dar es Salaam. Baada ya Malawi kutangaza kujitoa katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka kati yake na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa, Serikali imeitaka nchi hiyo kuacha kutapatapa na kamwe isithubutu kugusa eneo hilo la mpaka.
Imesema kama nchi hiyo itakiuka, Serikali ya Tanzania itaomba ushauri wa nini cha kufanya kutoka kwa jopo la usuluhishi wa sakata hilo linaloundwa na marais wa zamani barani Afrika, Festus Mogae (Botswana),Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Joachim Chissano (Msumbiji) ambaye ndiye mwenyekiti.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema, “Nadhani watasikia na kuelewa, Serikali ya Malawi iache kutapatapa, nchi zote ilikoenda kulalamika kuhusu mgogoro huu, Tanzania tumekuwa tukielezwa na hata hao wanaotueleza wanaishangaa sana Malawi.”
Kauli hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada ya Rais wa Malawi, Joyce Banda kusema kuwa mgogoro huo sasa utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia zimeshindikana.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam ambapo zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Katika maelezo yake, Rais Banda alisema nchi yake imejitoa katika mazungumzo ya usuluhishi kwa madai ya kuhujumiwa na Katibu wa jopo hilo ambaye ni Mtanzania, John Tesha kwa maelezo kuwa anavujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo.
Akitoa ufafanuzi wa kina juu ya mgogoro huo Membe alisema hilo lilionekana na ndiyo maana ulitolewa uamuzi kwamba nafasi ya Tesha itachukuliwa na Leonard Simao ambaye ni waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Msumbiji.
“Mwanzo walisema kuwa Tanzania tunataka kuwavamia, tukatoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo, baadaye wakaibuka tena na kusema kuwa tumetengeneza ramani ili kubadili eneo la mpaka, pia tulitoa ufafanuzi kuwa ilikuwa mipaka ya nchi na sasa wamekuja na jambo jingine. Novemba 17 mwaka jana tulikubaliana na hiki wanachokifanya Malawi ni kinyume na makubaliano. Ninawaomba waheshimu makubaliano yetu, hata kama jopo likitoa uamuzi wa kesi kupelekwa ICJ, Tanzania hatutakwenda mpaka tukutane na Malawi. Sasa kwa nini wao wanatapatapa?” alihoji Membe.
Alisema kuwa tangu kuibuka kwa mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika katika nchi za Uingereza, Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Huku akizungumza kwa ukali Membe alisema; “Wakati tunasubiri jopo lifanye kazi yake tunaiomba Malawi isiguse eneo la mpaka katika Ziwa Nyasa, na iwe hivyo hadi jopo au ICJ itakapotoa uamuzi.”
Mgogoro ulivyoanza
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania ilitoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni kutafuta mafuta katika eneo la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
|
0 Comments