Kenyatta ataiga mfano wa Rais Barack Obama wa Amerika, alipoapishwa hadharani mjini Washington DC mnamo Januari 21, 2013, ambapo aliomba mkewe Michelle Obama amshikie Biblia.
Siku hiyo Rais Mwai Kibaki atamkabidhi katiba mpya Kenyatta, ambayo ilianza kutumika mnamo Agosti 2010. Mtindo huu utakuwa wa kwanza tangu nchi hiyo kupata Uhuru. Sherehe hiyo itafanywa katika Uwanja wa Michezo wa Moi Kasarani, ambapo pia Naibu wa Rais William Ruto ataapishwa.
Shughuli hiyo inatarajiwa kumalizika saa 7.45. Kamati ya Mamlaka ya Ofisi ya Rais tayari ina ratiba ya mpangilio wa shughuli hiyo.
Ratiba hiyo ina picha ya rais anayeondoka katika ukurasa wa pili na ya Kenyatta katika ukurasa wa tatu. Kamati hiyo imeteua Rais Yoweri Museveni kuzungumza kwa niaba ya wageni wote waalikwa siku hiyo.
Hapo jana asubuhi, kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Kimemia, ilisema kwamba shughuli itaanza rasmi 5:45 asubuhi Rais Kibaki atakapowasili uwanjani.
Kulingana na mpangilio uliopo, wageni watahitajika kusimama Rais Kibaki akiwasili, wakati wa sherehe ya kuapishwa, saluti ya mizinga 21 itakapopigwa nje ya uwanja na wimbo wa taifa utakapoimbwa kabla ya Rais Kibaki na rais mpya kuondoka uwanjani.
Siku hiyo, Kenyatta atapambwa kwa vifaa vya mamlaka ambavyo ni pamoja na Mkuu wa Nakshi (CGH), pia atapokea mkuki, ngao na katiba.
Zana hizo zinaashiria mamlaka; kwa mfano Katiba inasimamia Kenya na watu wake, mkuki unasimamia Amiri Jeshi Mkuu ilhali CGH ni heshima kubwa zaidi Kenya.
0 Comments