Kwa kuanza ni vizuri tukatupa jicho letu katika haki za msingi za mtuhumiwa wa kosa au makosa ya jinai pindi anapokamtwa na polisi.
Kuna mambo kadhaa unayotakiwa uyajue, ambayo mtuhumiwa wa kosa la jinai anatakiwa afanyiwe wakati wa kupekuliwa au kukamatwa.
Kwanza, kumkamata mtuhumiwa kunaweza kuwa kwa kutumia hati ya kumkamata au inaweza kufanyika bila kutumia hati ya kumkamata.
Kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, iwapo mtuhumiwa atakuwa ameshafunguliwa mashitaka, basi mahakama kwa kutumia hakimu wake itamuita kwa kutumia hati ya kumkamata mtuhumiwa huyo na kama mtuhumiwa huyo atakuwa hajafunguliwa mashitaka kabla hajakamatwa, basi samansi itatumika na wakati mwingine mtuhumiwa anaweza kukamatwa bila hata kutumia hati ya kukamata.
Kumkamata mtuhumiwa bila kutumia hati ya kukamata kunaweza kufanywa na mtu yeyote, si lazima ofisa wa polisi kama ambavyo kifungu cha 16 na 14 cha sheria hii kinavyotamka bayana.
Miongoni mwa watu ambao pia wanaweza kumkamata mtuhumiwa wa kosa la jinai ni pamoja na hakimu wa mahakama yoyote iliyowekwa kisheria, walinzi wa amani, yaani wajumbe wa nyumba kumi/mabalozi wa nyumba kumi na ofisa watendaji wa kata na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa.
Hata hivyo, watu hawa watamkamata mtuhumiwa ikiwa tu kama mtu huyo atakuwa anafanya kosa la jinai lililo ainishwa chini ya kifungu cha 18 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Kimsingi ni jukumu la ofisa wa polisi au mtu yeyote anayemkamata mtuhumiwa, kumtaarifu mtuhumiwa huyo sababau ya kumkamata na si kumkamata kiholela kama ambavyo wakati mwingine inafanyika.
Hali hii wakati mwingine inasababisha watuhumiwa kukataa kukamatwa na hivyo kuleta mtafaruku baina yao na mtu/watu wanaoenda kutimiza wajibu wao wa kisheria kuwakamata watuhumiwa hao.
Hiki ni kigezo muhimu cha kisheria kwa watu wanaokwenda kuwakamata watuhumiwa wao kukitimiza kabla ya kuwakamata.

Kwa upande wa watu wasio askari wanaokwenda kuwakamata watuhumiwa, inawalizimu kuwakabidhi watuhumiwa hao katika mamlaka zinazohusika bila kuchelewa.
Na kwa mamlaka husika tuna maanisha ampeleke mtuhumiwa kituo cha polisi au mahakama iliyo karibu naye.
Hii ni muhumu kwa sabababu watu binafsi hawana nyenzo au mahala panakokidhi viwango vya kuwaweka watuhumiwa na zaidi ya yote kuna uwezekano mkubwa kwa wao kutozingatia kanuni na vigezo muhimu vya kisheria katika kuwahifadhi watuhumiwa wao.
Mfano mzuri tunaupata katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Dastur, A.L.R 421, ambapo mtuhumiwa aligoma kukamatwa kwa kutoambiwa sababu ya kukamatwa.
Zaidi ya hapo, mtuhumiwa alitoa kisu na kumchoma nacho askari mmoja wapo kati ya watatu waliokwenda kumkamata.
Mahakama baada ya kuridhika na maelezo yake, ilisema kwamba mtuhumiwa alikuwa na haki ya kuelezwa sababu ya kukamatwa.
Kitu kingine cha msingi ambacho unatakiwa kujua ni kwamba mtu anayetakiwa kumkamata mtuhumiwa ni kwamba anatakiwa kutotumia nguvu za ziada wakati wa kumkamata mtuhumiwa.
Hii inamaana kwamba, vitu kama pingu, kumshika mtu kibindo na kadhalika, vinatakiwa kutumika ikiwa tu mtuhumiwa mwenyewe atakuwa anakataa kukamatwa kihalali.
Hii ndiyo maana ya nguvu za ziada kama zilivyoelezewa chini ya kifungu cha 12 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Hata hivyo, suala la kuamua kama nguvu za ziada zimetumika au la, litaamulia kutokana na mazingira
ya kesi yenyewe.
Sheria hii pia imetoa mamlaka kwa polisi kuvunja nyumba ili kumkamata mtuhumiwa aliyejifungia ndani, kama ambavyo kifungu cha 19 na 20 cha sheria hii kinavyoelekeza.
Hii ni kwa sababu inawezekana kwa mtuhumiwa wa kosa la jinai akajifungia ndani ya nyumba au jengo ili akimbie mkono wa sheria.
Hivyo kwa kutambua hilo ndipo chini ya kifungu cha 20 cha sheria kikatoa msimamo huu.
Pamoja na hayo yote, sheria hii imekataza kitendo cha kuwakamata watoto au mke/mume wa mtuhumiwa kwa madhumuni ya kumshurutisha mtuhumiwa ajisalimishe katika mkono wa sheria.
Kwa upande wa kumpekua mtuhumiwa au nyumba yake, kitendo hiki pia kinaweza kufanywa kwa kutumia hati ya kupekua au bila hata kutumia hati ya kupekua.
Ndugu msomaji unatakiwa kujua kwamba kuna mazingira yanayoweza kumlazimisha askari kukupekua bila kuwa na hati ya kukupekua, na hii mara nyingi hutoke pale ambapo suala lililokuwepo ni dharura.
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pia imeiingiza dhana hii katika vifungu vyake. Hata hivyo, mtu mwenye jinsia ya kike ni lazima apekuliwe na mwanamke mwenzake na hivyo hivyo kwa mwanaume ambaye naye ni lazima apekuliwe na askari mwenye jinsia ya kiume.
Hii ni katika kulinda heshima na utu wa mtuhumiwa anayepekuliwa.
Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha sheria hii. Kitu cha msingi kuhusu kupekuliwa ni kwamba, kwa mujibu wa sheria, mtu anatakiwa kupekuliwa kati ya mchana hadi jioni, yaani kipindi ambacho jua linachomoza na pale jua linapokuchwa tu, na si vinginevyo.
Kwa maneno mengine ni kwamba mtuhumiwa haruhusiwi kupekuliwa wakati wa usiku isipokuwa kama mahakama imeruhusu hivyo chini ya kifungu cha 40 cha sheria hii.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai yaani ‘Criminal Procedure Act’ inaeleza wazi kuwa mhalifu aliyeko kizuizini ni lazima apewe haki zake za kimsingi na kuthaminiwa kama binadamu.
Utu na heshima ya kila mtu lazima vizingatiwe. Huduma kama za afya, ushauri, chakula na malazi ni muhimu kuzingatiwa, ni lazima huduma hizo zitolewe kila mara zinapoombwa au kuhitajika.
Hata wewe unaweza kuwa shahidi wa vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya polisi au walinzi wengine wa amani.
Mfano mzuri ni pale mhalifu anapokamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi, kama kawaida polisi huwaamuru kuvua mikanda, viatu na kuwanyang’anya vitu vingine vyote vya thamani kama pochi na simu.
Sheria ipo wazi kabisa kuhusu mtuhumiwa ambaye yupo kizuizini, ni haki yake kwanza baada ya kugundua atakuwa kizuizini ni lazima aweze kuwataarifu ndugu zake kuwa yeye amewekwa kizuizini, au apewe nafasi ya kuwasiliana na mwanasheria wake au wanasheria wake.
Kama mtuhumiwa huyu mara afikishwapo kwenye kituo cha polisi/ kizuizini na kunyang’anywa kila kitu ikiwamo simu yake, je, atawezaje kupewa nafasi ya kuwasiliana na hao ndugu zake au wanasheria wake?
Angalau basi simu za ofisini zitumike ili kuwapelekea ndugu zake taarifa kuwa fulani amekamatwa na anatuhumiwa kwa kosa fulani.
Kwa upande mwingine, sheria inampa mamlaka polisi kutompa ruhusa mtuhumiwa huyo ya kuwasiliana na ndugu zake au jamaa zake kwa kuhofia endapo mtuhumiwa huyo atapewa nafasi kama hiyo kwa kupitia ndugu zake au jamaa zake, anaweza kupoteza ushahidi wa kosa lake, au kwa kumruhusu tu kunaweza kusababisha mtuhumiwa huyo kutoroka kutoka kizuizini.
Kama polisi atakuwa na sababu nilizozitaja hapo juu, basi anaweza akakataa mtuhumiwa kuwasiliana na ndugu zake, tofauti na sababu hizo endapo polisi amekataa kumpa ruhusa mtuhumiwa huyo basi atakuwa hajamtendea haki kama ilivyooneshwa katika sheria.
Kama mtuhumiwa hana simu au jinsi ya kutoa taarifa kwa nduguze au wanasheria wake, basi sheria inasema polisi wafanye juhudi kutafuta vyombo kama hivyo kumrahisishia mtuhumiwa kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa zake popote pale walipo.
Vile vile ikumbukwe kwamba wakati polisi wanaandaa taarifa ya mtuhumiwa ni lazima wairudie kwa kuisoma mbele ya mtuhumiwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho, na kumuuliza mtuhumiwa kama au endapo kuna kitu kimeachwa au kuna marekebisho mengine, hii nayo ni hatua ya muhimu sana kabla mtuhumiwa huyo ajaweka saini yake.
Ninachoweza kusema zaidi, polisi na raia wawe na kiu ya kuzifahamu sheria zinazowaunganisha na kama wanazifahamu basi wazifuate ili kuondokana na uonevu ambao mara nyingi wanalalamikiwa polisi.
Kwa hili, nadhani hakuna njia ya mkato zaidi ya kufuata sheria halali za nchi yetu.Ikumbukwe kwamba polisi si mahakama ambayo inaweza kutoa hukumu, wanachoweza kukifanya polisi ni kuhakikisha wanafanya kila waliwezalo kumpeleka mtuhumiwa mbele ya mahakama pamoja na kukusanya ushahidi wa kutosha.
Mahakama kisheria ndiyo chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kusikiliza na kupitia ushahidi wote na kuhakikisha kwamba mtuhumiwa ana hatia au hana.
Mahakama baada ya kuchambua kwa kina ushahidi na vidhibiti vyote vilivyotolewa na polisi pamoja na ule uliotolewa na mashahidi, itaendelea kutoa uamuzi wake kwamba mtuhumiwa ana hatia.