Bendi ya Skylight ikiwa kazini.
KUHUSU SKYLIGHT BAND Akizungumzia madai ya Jide kunyang’anywa wanamuziki wake na kupelekwa Skylight, Ruge alikanusha vikali akisema yeye binafsi wala Clouds si wamiliki isipokuwa ni ya Sebastian Ndege. “...lakini wanamchukulia wasanii, yeye anatafuta wengine anawatengeneza, wananyanyuka na bendi inaendelea kuwepo. Ndiyo maana anaitwa Iron Lady, ni sawa kabisa. Jaydee anatakiwa kukubali ushindani wa kibiashara.”
ATUPA KOMBORA Katika mahojiano hayo, Ruge alikwenda mbali zaidi akisema kwamba, Jide yupo katika vita ya ushindani wa muziki lakini kwa bahati mbaya ameelekeza nguvu zake sehemu isiyostahili.
“Jaydee yupo kwenye anguko la muziki na kusema kweli, anasumbuliwa na Skylight Band sasa yeye anapigana the wrong way (isivyo), namshauri aelekeze nguvu zake Skylight. Apambane na washindani wake ili aendelee kuwa juu. Akubaliane na changamoto za kibiashara. Apigane kimuziki aendelee kusimama,” alisema.
SI SUALA LA KITAIFA Alisema haoni kama ni sahihi suala la Jide kukuzwa kwa kiwango hicho kuwa kama la kitaifa kwa sababu ni jambo binafsi la kibiashara ambalo linaweza kumalizwa kwa mazungumzo. Alitoa mfano kwamba, mgahawa wake wa Nyumbani Lounge umempiga marufuku Sam Machozi kufika pale kwa sababu amekwenda kinyume na taratibu za mgahawa huo. “Mbona hilo halikuwa la kitaifa? Kuna wakati fulani nyimbo za Ray C (Rehema Chalamila) zilipigwa marufuku EATV, ilibidi mimi niongozane na Ray C hadi kwa mzee Mengi (Reginald) kumuombea msamaha ndipo nyimbo zake zikaachiwa. Mbona hilo halikuwa la kitaifa? Haya ni mambo binafsi na yanaweza kumalizika bila kukuzwa,” alisema.
AKUBALI KUKUTANISHWA Katika kuonesha kwamba yupo tayari kukutana au kukutanishwa na Jide na kuyamaliza, Ruge alimtaka msanii huyo kutumia njia iliyo sahihi kumaliza tatizo lililopo kati yake na wao (Clouds) au yeye binafsi. Alisema: “Sisi hatupigi nyimbo zake kwa sababu ametukosea lakini kama anahisi sisi ndiyo wakosaji kama anavyosema, zipo njia za kufanya ili kutafuta utatuzi. Jide anajua cha kufanya. Sisi hatuna matatizo naye. Kama anataka kuendelea kufanya kazi na sisi hata kesho au keshokutwa anaweza kuja tukazungumza. “Si lazima aje yeye, anaweza kutuma hata watu anaowaheshimu, tukakodi mahali pazuri tukakaa na kuzungumza. Haya malumbano hayasaidii muziki wetu. Jaydee aje na hoja kamili zilizoainishwa tuzungumze. Nasisitiza haya ni mambo binafsi na si ya kitaifa.”
ASITISHA BONGO FLEVA Katika kuonesha kuwa kila taasisi huwa na miongozo yake, Ruge aliagiza mara baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo, redio isipige kabisa nyimbo za Bongo Fleva kwa siku nzima kama mfano wa uamuzi wa mamlaka ya taasisi yao. “Ni utaratibu tu, ndiyo maana kuna siku huwa tunaamua kupiga nyimbo za wanawake tu. Sasa leo nasema kuanzia muda huu, msipige Bongo Fleva hadi atakapotoka Dj Nelly alfajiri. Hili ni agizo,” alisisitiza.
JIDE BADO YUPO NGANGARI Katika kuonesha kuwa maneno ya Ruge hayakumwingia Jide, muda mfupi baada ya kauli hiyo kuisha aliandika katika akaunti yake ya Facebook kwamba mpambano bado unaendelea na ameahidi ataeleza mengine mazito zaidi hapo baadaye.Jide aliandika: “Kama mtakumbuka niliahidi kutoa awamu ya pili tar 15 au 17 Mei na ahadi ni deni... japo naona mbali ila nitafanya hivyo. Bado nina mengi sana ya kuzungumza kuhusu Ruge na wenzake... Ile ilikuwa ni trailer tu, movie ndiyo inaanza sasa...”
MEZANI KWA MHARIRI Ni vyema Jide akafikiria vizuri suala hili; maadam upande mmoja upo tayari kukutana naye akubali kufanya hivyo ili kumaliza tofauti hizi na kuendelea na ujenzi wa taifa. |
0 Comments