Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mawakili wa watuhumiwa hao kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kuwafutia kesi na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi yenye mashtaka hayohayo kwenye Mahakama ya Kisutu, Machi 20, mwaka huu.
Jaji Kaduri alikubaliana na hoja za Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza alizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kuwa uamuzi wa DPP ulikuwa sahihi.
Lwakatare na Rwezaura walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na kusomewa mashtaka hayo manne katika kesi namba 37 ya mwaka 2013.
Zombe aachiwa huru
Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na wenzake wanane.
Hata hivyo, mahakama hiyo imetoa fursa nyingine kwa DPP kukata rufaa nje ya muda kwa kuzingatia Sheria ya Ukomo wa Muda.
DPP alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi mmoja wa Manzese, Dar es Salaam.
Mahakama hiyo iliitupilia mbali kutokana na kasoro za kisheria zilizobainika katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Kasoro hiyo ni kuandika kuwa hukumu inayopingwa ilitolewa na Jaji Salumu Massati wa Mahakama ya Rufani, badala Jaji wa Mahakama Kuu.
0 Comments