Mishahara
Rais Kikwete alisema kuwa katika bajeti hiyo, Serikali itatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma na sekta binafsi huku akiahidi kuwa italingana na hali halisi ya maisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imetenga zaidi ya Sh4.76 trilioni katika Bajeti ya Mwaka 2013/14 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi wa umma.
Alisema katika Bajeti hiyo, asilimia 44.9 ya fedha itakuwa kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi, fedha ambazo zitatoka katika vyanzo vya mapato vya ndani.
Alisema katika kiasi hicho, zaidi ya asilimia 4.9 zinatoka kwenye mapato ya Serikali na kilichobaki kitatoka kwenye vyanzo mbalimbali.
“Tunajua kuwa, mishahara ya wafanyakazi ni midogo, lakini Serikali imekuwa ikijitahidi kuongeza kila mwaka ili iweze kuendana na hali halisi ya maisha,” alisema.
Alisema mwaka juzi, kima cha chini kilikuwa Sh65,000 ambacho kiliongezwa hadi kufikia Sh125,000 na kwamba mwaka huu wataongeza kiasi kikubwa ili kiweze kukidhi mahitaji.
Mifuko ya Jamii
Akizungumzia kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Rais Kikwete aliwaondoa hofu wananchi na kusema iko hai na wafanyakazi watakaostaafu watalipwa mafao yao kama kawaida.
Alisema utafiti uliofanywa hivi karibuni na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), umebaini kuwa mifuko hiyo haina matatizo yoyote.
Alisema Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), ulikuwa na matatizo ambayo yalianza kabla ya mwaka 1999, jambo ambalo lilifanya uwe na madeni ya zaidi ya Sh6 trilioni. Baada ya kuona hivyo, alisema Serikali iliweka utaratibu wa kuuchangia kiasi cha Sh50 bilioni kila mwaka katika mapato yake.
Alisema kutokana na hali hiyo fedha hizo ndizo zinazotumika kulipa wafanyakazi na wastaafu mafao yao na kwamba mpaka sasa hakuna aliyelalamika kutolipwa mafao yake.
“Naomba niwaondoe hofu Watanzania wenzangu. Hakuna mfanyakazi atakayekosa kulipwa mafao yake pindi anapostaafu katika mifuko ya hifadhi ya jamii ukiwemo PSPF,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa uwekezaji katika mifuko hiyo unakua siku hadi siku.
Rais Kikwete aliwashauri waajiri kuwaacha wafanyakazi wajiunge na mfuko wowote wanaotaka ili waweze kuhifadhi mafao yao.
0 Comments