Dodoma.
 Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mwanamrisho Taratibu Abama jana alianguka ghafla katika Viwanja vya Bunge wakati akijiandaa kuhudhuria semina ya wabunge ya kujadili rasimu ya Sera ya Gesi asilia.
Mapema asubuhi mbunge huyo alionekana katika Viwanja vya Bunge kabla semina kuanza, lakini ghafla alianza kujisikia vibaya.
“Mheshimiwa leo (jana), alifika kama kawaida, lakini ghafla alisema hajisikii vizuri, hivyo tulimshauri akae chini kwanza kabla ya kwenda katika semina,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa Bunge ambaye hakutaka kutaka jina lake.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, mbunge huyo baada ya kukaa kwa muda alianza kuishiwa nguvu na kuanguka ndipo wafanyakazi wa Bunge walipomsaidia kwa kumpeleka katika Zahanati ya Bunge.
Baada ya mbunge huyo kuingia katika chumba cha daktari alipewa huduma ya kwanza na kutundikiwa ‘dripu’ kabla ya kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa Dodoma.

Waandishi wa gazeti hili walimshuhudia mbunge huyo akiwa na maumivu makali wakati alipobebwa kwenye machela na kutundikiwa ‘dripu’.

Tukio hilo lilotokea saa 5.30 asubuhi na kusababisha baadhi ya wabunge na wafanyakazi kupigwa butwaa.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema; “Ndiyo kwanza nimefika na mimi nimezisikia habari hizo, lakini bado sijapata taarifa rasmi.”
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Dodoma, Zainabu Chaula alithibitisha mbunge huyo kupokewa hospitalini, lakini alikataa kueleza kinachomsumbua kwa maelezo kuwa ugonjwa ni siri ya mhusika.

Mapema Machi mwaka huu, mbunge wa Chambani Salim Hemed Khamis (CUF), alianguka alipokuwa akihudhuria vikao vya Kamati za Bunge katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam. Mbunge huyo alipelekwa hospitali kwa matibabu, lakini baadaye alifariki dunia.

Aidha, Aprili 14 mwaka jana, mbunge wa Viti Maalumu (CUF) Clara Mwaituka alianguka ghafla alipokuwa akihudhuria vikao vya Bunge mjini Dodoma, ambapo alipatiwa matibabu na kupona.