“Halafu lazima watu wajue kuwa nchi hii ni yetu sote, kama ni kubanana lazima tubanane humuhumu, lakini kwa idadi ya wingi wa watu isiwe mbanano wa mapanga,” aliongeza Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema vurugu zinazotokea zinafanywa na watu wachache ambao hawana mamlaka katika taasisi za kidini, na aliwataka viongozi wa dini zote kukemea vurugu, kuihubiri amani na kuwakumbusha waumini wao kuipenda nchi yao.
Alirudia kauli yake kuwa Serikali haitawavumilia watu wanaoendelea kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio cha masuala ya dini.
“Dini zote zinahimiza upendo, hakuna dini inayohubiri kuuana, ukiona dini inayohubiri kuuana hiyo itakuwa ni ya shetani, dini ya kweli inahimiza upendo kwa kila mtu,” alisema Rais Kikwete.
Awali Askofu Mkuu aliyewekwa wakfu, Dk Chimeledya aliiomba Serikali kushughulikia changamoto za nchi ikiwamo suala la umaskini, maradhi, ujinga na hatari ya kuporomoka amani.
Dk Chimeledya alisema kuwa rushwa, dawa za kulevya, ufisadi na mauaji ya vikongwe ni miongoni mwa mambo yanayoiondolea sifa Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijulikana kama kisiwa cha amani.Aidha, Dk Chimeledya alizungumzia migogoro inayolikabili Kanisa la Anglikana Tanzania na kusema kuwa uongozi unapaswa uketi na kutafakari jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazosababisha mgawanyiko miongoni mwa waumini wa kanisa hilo.
0 Comments