Sir Alex Ferguson akiwaaga mashabiki katika Uwanja wa Old Trafford. |
Ferguson aliyeipa Man United makombe 13 ya Ligi Kuu England, aliwaaga mashabiki kwenye uwanja huo, lakini karibu dunia nzima ilishuhudia mechi hiyo muhimu na ya kihistoria.
Moja ya vitu alivyovifanya Kassam ni kuinua bango aliloliandika hivi: “Thank you Sir Alex, with love from Tanzania.” Kwamba: “Nashukuru sana Sir Alex, kwa mapenzi kutoka Tanzania.”
Bango hilo la Kassam ambaye baba yake Fazal Kassam aliwahi kuwa mweka hazina wa klabu ya Simba, lilizua gumzo kubwa katika mitandao. Ingawa wapo walioonekana kutopenda yeye kupongezwa, lakini wengi walifurahia na kusema wazi walitamani kuipata nafasi hiyo muhimu zaidi.
Championi: Hongera kwa nafasi hiyo, ulifanikiwa vipi kupata tiketi hiyo?
Kassam: Nashukuru, tuna kundi letu la marafiki ambao baadhi yao ni Watanzania na Wakenya, wao wanaishi hapa Uingereza. Wao ni Season Ticket Holders (wana ticketi za mwaka mzima kwenda Old Trafford game zote). Ndiyo nikanunua tiketi kutoka kwa mmoja wao kwa bei ya pauni 50 (Sh 123,929).
Upatikanaji wa tiketi kwa mechi kama hizi ni ngumu sana kwa kweli, tiketi ziliuzwa dola 5,000 (Sh milioni 13) kwenye intaneti na uwanjani ziliuzwa hadi dola 1,000 (Sh milioni 1.6), dakika za mwisho. Nawashukuru sana marafiki zangu kwa bei waliyonipa kupata tiketi hiyo.
Championi: Hiyo ni mara yako ya kwanza Old Trafford?
Kassam: Tangu nilipokuwa mdogo, nilikuwa na ndoto ya kwenda OT siku moja na kukutana na angalau Ferguson. Tangu nimekuja huku kusoma mwaka 2011, nimeshawahi kufika kama mara nane hivi, ikiwemo katika mechi dhidi ya Liverpool na ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Madrid.
Championi: Hali ilikuwaje njiani wakati wa kwenda uwanjani?
Kassam: Kuanzia asubuhi, redio, runinga, kwenye mitandao yote ishu ilikuwa ni mechi hiyo ya Ferguson kuaga. Tukiwa njiani tulipishana na gari nyingi zenye bendera za Manchester United. Kusema kweli, Tanzania tuko mbele zaidi kwenye kushangilia hasa tunapokuwa tunakwenda uwanjani katika mechi.
Wao naona wametuzidi wanapokuwa wameingia uwanjani, maana hapa, njiani huwa huoni fujo sana, lakini ukikaribia uwanjani unasikia nyimbo tofautitofauti zikiimbwa. Tofauti moja kubwa ambayo ninapenda sana sisi Watanzania tuifanyie kazi, ni jinsi ya ushangiliaji katika viwanja vya huku. Wanaimba nyimbo za aina tofauti, watu wanashangilia mwanzo mwisho na pia huwa watulivu na wenye heshima sana.
Championi: Ulipoingia uwanjani, nini ulikiona ni tofauti ukilinganisha na hapa nyumbani?
Kassam: Kila kiti kilikuwa na bendera ya Champions 20, ila mimi sikuchukua bendera, bali nikaonyesha bango langu, ndipo watu walipogeuka na kunishangaa, wengine wakichukua picha na kunipigia makofi. Kuanzia pale ndipo watu wa runinga, wapigapicha, walikaribia kwangu na kuchukua picha.
Championi: Kulikuwa na Watanzania wengine?
Kassam: Niliowaona mimi ni wawili, pamoja na mimi, Wakenya walikuwa wanne na hili ndilo kundi tulilokwenda nalo pamoja uwanjani. Ila pale uwanjani niliketi karibu na mtu kutoka Urusi na wengine kutoka Hispania, Waingereza na wengine ambao sikuweza kutambua uraia wao.
Championi: Vipi hukupata hata bahati ya kumsogelea Ferguson?
Kassam: Uwanjani nilikuwa karibu na Ferguson, tukiwa na umbali wa viti kama 10 hivi kushoto kwangu. Tuliruhusiwa kusimama na kuchukua sahihi yake, ila nilichelewa kwa sababu tulikutana na foleni ndefu. Baada ya kuchukua kikombe, alipita karibu nasi kabisa, nikamuona kwa karibu.
Championi: Ilikuwaje kwa mashabiki baada ya hotuba yake?
Kassam: Baadhi ya watu walimwaga machozi waliposikia hotuba ya Ferguson. Kwa kweli, kuna wengi waliokuwa na huzuni kuona Ferguson akistaafu.
Championi: Kama unapenda soka, hapa nyumbani ni shabiki wa timu ipi?
Kassam: Nyumbani Tanzania ni shabiki mkubwa sana wa Simba Sports Club, huwa nakwenda mara nyingi sana uwanjani, pia kuna wachezaji wa Simba ni rafiki zangu. Nakukumbusha pia, Simba iko katika familia yetu maana baba yangu mzazi, Fazal Kassam alikuwa mweka hazina wa Simba enzi hizo kipa alikuwa ni Mohammed Mwameja.
Kassam alisema alikuwa katika maandalizi ya kuiwahi mechi kati ya Yanga na Simba iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
0 Comments