Mbunge wa Arusha,Godbless Lema 

Arusha.
Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema, amewaonya wagombea udiwani wa chama hicho, katika kata nne jijini la Arusha, kuacha kutoa ahadi zisizotekelezeka katika kampeni zao.

Akizungumza katika kampeni zilizofanyika Kata ya Elerai jana, Lema ambaye anaongoza kampeni za Chadema kwa sasa katika kanda ya Kaskazini, kabla ya timu ya viongozi wengine wa kitaifa kufika, alisema ni heri kutokupata kura kuliko kuwadanganya wananchi kwa kutoa ahadi za uongo.

Lema pia aliwaonya wagombea hao, kuacha kuomba kura kwa misingi ya udini, ukabila ama ukanda kwani, hakuna mgombea ambaye anaweza kushinda kwa kuungwa mkono na dini moja au kabila moja pekee.

“Hakuna kosa kubwa kwa sasa katika siasa kama kuomba kura kwa udini au ukabila, mkifanya hivyo mtapotea na sisi hatutawaunga mkono,” alisema Lema.
“Ukweli unadumu daima, kama kuna watu wanasema hawakuchagui hadi uruhusu biashara ya mirungi au uwape mkopo wa kupika gongo, bora wasikuchaguwe kabisa,” alisema Lema.

Alisema wagombea hao, kama wakitoa ahadi za uongo, watasababisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uwe mgumu kwa chama hicho kwani hawataweza kutimiza ahadi.

“Hatutaki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uwe mgumu kwetu, mimi mwaka 2005 nilishindwa kwa kukataa kutoa ahadi za uongozi, lakini mwaka 2010 nimechaguliwa kuwa mbunge yale walioahidi wenzangu walishindwa kutekeleza,” alisema Lema.
Katika kampeni hiyo, mgombea wa udiwani wa Chadema katika kata ya Elerai, Jeremiah Mpinga, aliomba wakazi wa kata hiyo, kumchagua kwani anajua matatizo yao.

Hata hivyo, Mpinga anakabiliwa na upinzani mkali katika kata hiyo, toka kwa mgombea wa udiwani wa CUF, John Bayo ambaye alikuwa ni mmoja wa madiwani watano wa Chadema waliofukuzwa uanachama.

Bayo ambaye amekuwa akiungwa mkono na makundi ya watu wa kati hasa kutokana na misimamo yake, alisema jana kuwa ana uhakika wa ushindi na kurejea katika halmashauri ya jiji.

“Nia yangu kubwa ni kurejea katika halmashauri kwa tiketi ya CUF ‘‘ alisema.