Na Hamida Hassan INAUMA sana! Staa wa maigizo ya runingani na filamu za Kibongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ amepata pigo kubwa la mama yake mzazi aitwaye  Mwadodo Ramadhan maarufu kwa jina la ‘Bi. Dodo’ kukata roho mikononi mwake akiwa anamkimbiza hospitali kwa ajili ya kuokoa uhai wake, Amani lina habari ya kusikitisha SEHEMU YA TUKIO
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mama huyo aliaga dunia ghafla usiku wa kuamkia Jumanne wiki hii akiwa ametolewa nyumbani kwa mwigizaji huyo, Ilala-Bungoni na kukimbizwa Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam.
“Dude alikuwa akiishi na mama yake mzazi licha ya kwamba hapa Dar ana ndugu wengine, mpaka mauti yanamkuta alikuwa akiishi nyumbani kwake na siku ya kifo alikuwa akimuwahisha hospitali ya Amana,” kilisema chanzo.

ALIJUA MAPEMA ATAKUFA, AFANYA MAAJABU
Kwa mujibu wa chanzo hicho, siku moja kabla ya kifo cha mama huyo, yaani Jumatatu, marehemu alitembea sana. Alisema marehemu alikwenda sehemu mbalimbali za Jiji la Dar wanazoishi watoto wake wengine kwa lengo la kuwajulia hali, jambo ambalo ni kama la ajabu kwani siku za nyuma hakuwa mtu wa kusema anawatembelea watoto wote kwa siku moja.

“Inashangaza sana na naweza kusema ni ajabu kwani siku ya Jumatatu mama alimuaga mwanaye Dude kwamba anakwenda kuwasalimia ndugu zake wengine na angerudi jioni ya siku hiyohiyo, Dude akamkubalia na akampa nauli, akamwambia akawasalimie aendako,” kilisema chanzo.
Kikaendelea: Naamini kiroho marehemu alijua kifo kinamuita, sasa alikwenda kuwaaga watoto wake kwa vile hawataonana tena. Unajua mambo ya Mungu ni mengi sana, unaweza ukawa hujui lini utaondoka lakini ukafanya mambo yenye kuashiria kutambua kifo.

SIKU YA TUKIO
Kwa mujibu wa Dude, siku ya kifo cha mama yake, yaani Jumanne yeye hakuwepo nyumbani, alitoka kidogo, aliporudi alimkuta Bi. Dodo akiwa katika hali mbaya, jambo lililomshangaza sana.
“Mimi sikuwepo, niliporudi nikamkuta mama yupo katika hali mbaya sana wakati nilimwacha mzima kabisa, nikashangaa sana. Nilijaribu kumuuliza anaumwa nini, hakujibu kitu wala hakuonesha kuelewa chochote kile. Nilishtuka kidogo.
“Moyoni niliamini amepoteza fahamu tu kutokana na hali aliyokumbana nayo. Ilibidi tumkimbize Hospitali ya Amana ili madaktari wakampime na kugundua nini kilimsibu ghafla wakati alikuwa mzima wa afya. Mpaka hapo nilikuwa najipa moyo kwamba nakwenda na mama lakini nitarudi naye.”
Alisema pia aliwasiliana na ndugu mbalimbali wakiwemo wale waliotembelewa jana yake ili kuwajulisha kuhusu hali ya Bi. Dodo.

WAFIKA AMANA, MADAKTARI WANENA
Alisema walipofika Hospitali ya Amana, madaktari walimpima kwa vipimo vya kitaalam na kubaini kuwa mama Dude alishakata roho muda mfupi uliopita.
Walisema huenda mama huyo alikumbwa na mauti akiwa ndani ya gari kupelekwa hospitalini hapo ambapo Dude mwenyewe ndiye aliyemshika mama yake ndani ya gari hadi Amana.

KWA MUJIBU WA WATAALAM
Jumanne hiyohiyo, Amani lilizungumza na daktari mmoja (jina linahifadhiwa) wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhusu matatizo yanayowapata watu ghafla na kupoteza fahamu ambapo alisema:
“Mara nyingi ni mshtuko wa moyo, hasa nyakati za usiku. Hii huwapata watu wenye umri mkubwa kidogo au wale wenye msongo wa mawazo. Hali hii ikimpata mtu na akikata kauli hawezi kukaa sawa tena.”

KILIO CHA DUDE
“Sikujua kama nitampoteza mama yangu kwa siku hii (Jumanne) kwa sababu hakuwahi kunilalamikia kuhusu kuhisi maumivu yoyote yale,” alisema Dude.
Akaongeza: Naumia sana, siamini lakini najua imeshatokea, sina la kufanya, mama yangu hayupo tena duniani.
Alisema anamuombea mama yake afike salama safari yake hiyo kwani ameondoka ghafla na hakuwa akisumbuliwa na ugonjwa wowote, akaongeza ni mipango ya Mungu hivyo hawezi kumlaumu.
Marehemu Bi. Dodo alitarajiwa kuzikwa jana  (Jumatano), saa 10:00 kwenye Makaburi ya Ilala baada ya taratibu zote
kufanyika.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.