Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kuhusisha wasomi na wafuatiliaji wa mambo ya jamii nchini, unaonesha kuwa ipo mikono ya watu inayosababisha ghasia kuongezeka.
Usiku wa juzi, (Jumatano) wanajeshi wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walipoteza maisha na wengine 20 kujeruhiwa katika ajali ya gari wakiwa safarini wakitokea Nachingwea kuelekea Mtwara kutuliza vurugu zilizokuwa zikiendelea.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mtwara, Edrwad Gontako alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ya askari wa JWTZ, 41KJ Nachingwea, akafafanua kuwa, majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.
Aidha, hadi juzi (Alhamisi) wakati gazeti hili likijiandaa kwenda mitamboni, ilifahamika kwamba, mwananchi mmoja wa Mtwara alifariki katika vurugu hizo na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati watu 45 walikamatwa katika ghasia hizo.
Hili suala ukilitazama kwa juujuu unaweza ukafikiri tatizo ni gesi, siyo kweli. Kuna watu kwa manufaa yao wenyewe wanataka kuiharibu Mtwara ili isitawalike. Ni jipu la muda mrefu sasa ndiyo linatumbuka. Ukitafakari ishu ya gesi utagundua si jambo kubwa la kuharibu amani ya nchi yetu.
“Yapo masilahi ya watu fulani. Hili ni tatizo. Kinachoonekana sasa, hata kama serikali itaamua gesi ibaki Mtwara, bado litaibuliwa suala la bei ya korosho. Kwa ujumla kuna watu wanataka kuvuruga tu nchi,” alisema mmoja wa wasomi nchini aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Mwingine alisema: “Serikali ina mkono mrefu na siku zote hakuna mwananchi anayeweza kushindana na dola. Serikali yetu tunajua ipo makini na tunaisihi sana itumie nguvu na maarifa yote kuhakikisha inatuliza hali ya hewa iliyochafuka Mtwara. Siyo tu suala la gesi bali kuhakikisha hizi chokochoko zinazoletwa na watu kwa masilahi yao zinakwisha kabisa.”
0 Comments