Na Imelda Mtema HOST wa Shoo ya Wanawake Live inayoruka hewani kupitia Televisheni ya East Africa ‘EATV’, Joyce Kiria amewaacha watu hoi baada ya kutembea katikati ya Jiji la Dar, akimlilia muwewe Henry Kileo.

Joyce Kiria pamoja na watoto wake wakimlilia mumewe.

Kileo ni Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Mkoa wa Dar ambaye kwa sasa yupo nyuma ya nondo kwa tuhuma za kutajwa kwenye  tukio la kumwagiwa tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha katika uchaguzi mdogo wa Ubunge kwenye Jimbo la Igunga uliofanyika hivi karibuni.
Gazeti hili lilimnasa Joyce akiwa na wanaye wawili, Lincoln na Linston, msaidizi wake wa kazi za ndani ambaye hakufahamika jina na wadau wengine walioungana naye wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, kubwa wakitaka kujua mahali mumewe Kileo alipo.

Mume wa Joyce Kiria, Bw. Henry Kilewo, akiwa na watuhumiwa wenzake wa mashtaka ya Ugaidi yanayowakabili wakati walipofikishwa Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani Tabora kwa mara ya kwanza.

Joyce alisema, mumewe alikamatwa na kufikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Stesheni jijini, Ijumaa iliyopita ambapo alikuwa akimpelekea chakula lakini alipokwenda Jumamosi jioni, alielezwa kuwa mumewe huyo amehamishiwa kituo kingine lakini hakutajiwa.
“Siku aliyokamatwa (Ijumaa) nilimpelekea chakula mchana na jioni. Asubuhi yake yaani Jumamosi nikapeleka chai vizuri tu lakini niliporudi jioni kwa ajili ya kumpelekea chakula cha usiku, nikaambiwa amehamishiwa kituo kingine.

Joyce Kiria pamoja na wanafamilia wakiwa na mabango.

“Nikamuomba askari aliyekuwa zamu aniambie kituo alichohamishiwa lakini hakufanya hivyo, akasisitiza kwamba amehamishwa. Hii si haki jamani. Najua mume wangu anashikiliwa na polisi na yeye ni mtuhumiwa tu, sasa mimi kama mke wake ninapaswa kujua mahali mume wangu  alipo.
“Siwezi kukaa na hali hii ya mateso mimi na wanangu pamoja na dada yangu wa kazi bila kujua alipo mume wangu. Hapo sijatendewa haki, natakiwa niambiwe kituo alichohamishiwa ili nikamuone,” alisema Joyce.

Joyce akizidi kuuliza alipo mumewe.Baada ya mahojiano na gazeti hili, Joyce ambaye alipata wadau wengine waliokuwa wakiandamana naye, aliendelea kuzunguka kwenye mitaa mbalimbali ya katikati ya jiji, eneo la Posta wakiwa na mabango yao.