Maka Lombero akiwa amekaa kwenye ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, wiki hii. Picha na Ibrahim Yamola.
TOKA GAZETI LA MWANANCHI. 
Dar es Salaam. Kwa mtu uliyekutana naye miaka saba iliyopita wakati huo akiwa dereva wa magari makubwa aliyefanya kazi zake mchana na usiku huku akilazimika kunyanyua baadhi ya mizigo mizito, si rahisi kuamini kuwa mtu huyo leo hawezi hata kufungua mlango wa gari.

Huyo si mwingine bali ni Maka Lombero (39) mzaliwa wa Bukoba, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye anaishi maisha duni baada ya kukumbana na masahibu yaliyosababisha kukatwa kiungo kimoja baada ya kingine na kumwacha akiwa hana viganja vya mikono yote miwili na mguu wa kushoto.

Nilikutana na Lombero saa mbili na nusu usiku eneo la Kigogo Luhanga akiwa amekaa nje ya duka, huku ameengemea fimbo yake ya kutembelea. Nilipomsalimia alionekana ni mtu mwenye furaha asiye na wasiwasi wowote.Aliinua mkono wake uliokatika nusu na kuuelekeza kwangu akitaka nimsalimu kwa kumpa mkono.

Nilimpa mkono naye kwa furaha akaniambia: “Karibu ndugu yangu.” Huku akisogea niweze kukaa lakini kwa kuwa nafasi ilikuwa ndogo nilimwomba tuingie katika mgahawa uliokuwa karibu ili kuweze kuzungumza. Alichukua magongo yake ya kutembelea, kisha taratibu tukaingia ndani.

Alipoanza kunisimulia historia ya maisha yake ghafla furaha aliyokuwa nayo ilitoweka huku machozi yakimlenga. Kwa kuwa nilihitaji sana kujua historia ya maisha yake nilibadilisha mada kwa kumuuliza angependa kula chakula gani.
“Mimi situmii mayai, kama kuna viazi (chipsi) na mishikaki itanitosha,” alisema Lombero.

Wakati tukisubiri chakula alinieleza namna anavyokula; “Ndugu yangu, nina kula kama mbwa au paka. Ninaweka mdomo wangu kwenye sahani ya chakula na kuanza kula. Ni mateso tu niliyonayo,” anasema.

Anadokeza kuwa anahisi matatizo ya kuoza kwa viungo kulikosababisha akatwe mikono na mguu kunatokana na vitendo vya kishirikina alivyofanyiwa, baada ya kumpiga msichana mmoja ambaye aligombana naye katika mtaa wa TRM barabara ya Dodoma, Iringa mjini. “Kuna msichana tulipishana kidogo kauli akanipiga na tofali mgongoni, nilimpiga sana siku chache baadaye matatizo yalianza,” alifafanua.

Historia yake

Lombero anasema kuwa alihitimu elimu yake ya msingi mwaka 1988 huko Bukoba. Mwaka 1990 alijiunga na shule ya sekondari ya Mnazi Mmoja ya Jijini Dar es Salaam, aliposoma kwa miaka miwili na kuamua kuacha masomo kisha kwenda Tunduru kuchimba madini ya vito.

Mwaka 1995 familia yake ilimpeleka Morogoro kwenda kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Kihonda, ambako alifanikiwa kupata leseni ya kuendesha magari makubwa. Baada ya kuhitimu masomo alikaa mtaani kwa siku chache kabla ya kwenda Ifakara kwa baba yake ambako alipata kazi ya kuendesha lori katika kampuni ya Zaniri.

“Ile kampuni nilikaa nayo muda mfupi tu baadaye nilikuja Dar es Salaam nikapata kazi kwenye kampuni ya Mwarabu,” anasema na kuongeza kuwa kampuni hiyo alifanya nayo kazi muda mrefu ikilinganishwa na ile ya kwanza.
Baada ya kuacha kazi alikwenda Zanzibar kufanya kazi katika kampuni ya Zanzibar Cable, aliyodumu nayo kwa mwaka mmoja tu. Akiwa huko alifunga ndoa na Salima Lukas aliyezaa naye watoto wawili; mmoja wa kiume na mmoja wa kike.

“Tulipotoka Zanzibar, mwaka 2007 tulikwenda Iringa kwa wazazi wa mke wangu, tukiwa huko tukaanza biashara ya kuuza mkaa na huko ndiko ugonjwa ulipoanza,” alisema Lombero.

Matatizo yalivyoanza

“Nakumbuka ilikuwa ni saa tisa usiku nikiwa nimelala ndani ya kibanda kidogo cha udongo msituni tulikokuwa tunachoma mkaa, ghafla usingizi uliisha nikawa nahisi kuna watu wananipuliza, nilijaribu kuinuka lakini sikufanikiwa,” ndivyo anavyoanza kusimulia mkasa wake.
Anasema wakati akiendelea kutafakari kitu gani kinamtokea, ghafla kidole chake cha shahada (Ni kidole cha pili kutoka kidole gumba) cha kulia kilianza kuuma kama vile kuna mtu alimkanyaga.

“Nilipoangalia pembeni niliwaona watu watatu wamevaa ushungi wamesimama pembeni yangu sikuweza kuwatambua. Baadaye wale watu walitoweka.” Aliongeza.

Kuna mtu mmoja ambaye alikuwa akipita na baiskeli kila siku asubuhi na kumsalimia, huyo ndiye aliyemsaidia kumpa huduma ya kwanza kisha akampeleka kwa mganga wa kienyeji anayefanya kazi zake Ilula wilayani Kilolo.
“Mganga aliniambia kuwa kiganja changu kina chale tatu ambazo wakati wote huo nilikuwa sijaziona,” anasema na kuongeza kuwa: “Kwa kuwa nilikuwa na maumivu makali nilimsaidia kuziweka dawa kwenye chungu na kusogeza kuni kwenye moto ili anihudumie haraka maumivu yaishe.”

Baada ya dawa kuchemka kwa muda mrefu aliziweka juu ya mkono wake na kumwambia, kama atasikia maumivu yanakuwa makali zaidi asema ili waitoe dawa hiyo.

Kitu cha ajabu kilitokeo alipotoa zile dawa mkononi, ndani ya zile chale tatu vilitoka vipande vitatu vya vioo; viwili vya kijani na kimoja cheupe. Akamwambia aende nyumbani lakini arudi siku ya pili.

“Nilipofika home (nyumbani) nilikuwa mzima kabisa, nikamsimulia wife (mke) kusudi aamini ninachomwambia nikapiga ‘pushapu’ kadhaa, sikusikia maumivu kabisa,” alieleza.

Siku ya pili alipokwenda kwa mganga alipewa dawa, kama ilivyokuwa siku ya kwanza kitu kingine kikatoka katika zile chale, wakati huu kikatoka kipande cha mkaa. “Akaniambia niende tena siku ya tatu kwa sababu kuna kitu kibishi kinagoma kutoka,” aliongeza.
Alisema akiwa kwa mganga, huku nyuma mke wake alimpigia simu mama mzazi wa mume wake akimtaarifu hali aliyonayo mwanawe. Mama mzazi na mkewe walimzuia kurudi kwa mganga kwa madai kuwa anatapeliwa.

Maumivu kwenye kidole yalirudi kama yalivyokuwa mwanzo huku kidole kikibadilika rangi na kuanza kuwa cheusi. Asubuhi iliyofuata alipandishwa kwenye basi kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

Alipofika Dar es Salaam alipelekwa hospitali ya Kairuki kufanyiwa uchunguzi ambapo ilibainika kuwa mishipa inayopitisha damu kwenye kidole ilikuwa haifanyi kazi. Madaktari walijaribu kumpa tiba lakini akaanza kukata tamaa ya kupona. Ingawa madaktari walimwambia kuwa ugonjwa wake unatokana na sumu inayopatikana kwenye sigara, Lombero hakubaliani na matokeo ya matabibu hao japokuwa anakiri kuvuta sigara kwa miaka mingi.
“Wao wanasema sijui naumwa nini...mimi ninachojua hii ni michezo (ushirikina) tu nimefanyiwa, japokuwa ni kweli kwamba nimevuta sigara miaka 21 mfululizo kila siku nilikuwa navuta sigara kumi hadi 12,” alibainisha.

Kutokana na maumivi kwenye kidole kuwa makali, alikuwa akimwomba mtu yeyote aliyekaribu yake amkate kidole ili maumivu yaishe lakini wote walikataa.

Hata hivyo, hali ya kidole ilizidi kuwa mbaya madaktari wakaamuru kikatwe, ndipo alipopata nafuu na kurudi katika maisha yake ya kawaida huku akiwa amepoteza kidole kimoja.
Itaendelea wiki ijayo

Kwa mtu yeyote atakayeguswa na matatizo ya Lombero awasiliane naye au mke wake kwa kutumia simu 0753 042937

“Baada ya siku chache kidole cha mkono wa kulia kama kile kile kilichokatwa mkono wa kushoto kikaanza kuuma chini ya kucha, kikabadilika rangi taratibu na kuwa cheusi.” Alisema kwa uchungu kama vile maumivu bado yapo.

Hali ya kidole ilizidi kuwa mbaya kiasi cha kuwalazimu madaktari kukikata kidole hicho.

Baada ya miezi mitatu ugonjwa ulihamia katika mguu wa kushoto, kipele kidogo kikiambatana na maumivu makali kilitokea katika kidole cha mwisho. Siku mbili baadaye mguu ulianza kubadilika rangi, ngozi ikaanza kubanduka huku mguu ukikauka kutoka kwenye unyayo hadi juu kidogo ya goti.

Kutokana na ugonjwa kuhamia miguuni, baadhi ya ndugu walianza kuamini kuwa huenda ikawa ni imani za kishirikina kama ambavyo Lombero anaamini. Ndugu wakamshauri akamwombe msamaha yule mwanamke aliyempiga kule Iringa.
“Kwanza nilimtuma mke wangu aende kuniombea msamaha lakini yule mwanamke na mume wake walikataa wakisema hawahusiki na ugonjwa nilioupata, nikaamua kwenda mwenyewe,” alieleza.

Alisema alipofika nyumbani kwa huyo mwanamke, aliongea nao kwa muda mrefu na kutokana na hali aliyokuwa nayo walikubali kuhusika na ugonjwa wake na kumuahidi kuwa baada ya siku tatu angekuwa amepona ugonjwa wake.

Kinyume na matarajio yake siku hiyo usiku hali ilikuwa mbaya, maumivu yaliongezeka hakuweza kupata usingizi usiku kucha. Saa kumi na mbili asubuhi alipanda basi kueleka Dar es Salaam.

“Nilisafiri ninalia kama mtoto mdogo, kutoka Iringa hadi Morogoro nilimeza vidonge kumi vya dawa ya kutuliza maumivu aina ya ‘Diclopar’ lakini havikusaidia chochote,” alisema kwa uchungu.
Alipofika nyumbani kidole cha mguuni kilikuwa kimepasuka huku kikitoa damu nyingi. “Kutokana na maumivu niliyokuwa nayo siku ile shemeji yangu alidhani ningekufa, nilikuwa nalia sana.”

Siku iliyofuata alipelekwa hospitali ya Kairuki ambako alipewa barua ya kwenda hospitali ya Muhimbili alikolazwa miezi miwili, wakijaribu kuokoa kidole lakini hali ilizidi kuwa mbaya kiasi cha kuwalazimu madaktari kuukata mguu wa kushoto juu ya goti.
“Wakati nakatwa mguu sikuwa nasikia maumivu lakini nilisikia sauti wakati wanakata mfupa nikamuuliza daktari aliyekuwa karibu yangu ‘naona ndiyo mnakata mguu?’ “Ananiambia tulia wewe,” anaeleza kisha alianza kucheka.

Lombero alisema baada ya kukatwa mguu aliondokana na maumivu makali yaliyokuwa yakimsumbua, lakini aliendelea kukaa hospitali kwa muda wa mwezi mmoja zaidi hadi aliporuhusiwa kurudi nyumbani.

Madaktari waliwataka ndugu zake kuuchukua mguu uliokatwa na kwenda nao nyumbani kuuzika kitendo kilichosababisha ndugu kuwa na mawazo tofauti huku wengine wakitaka kuuchukua mguu huo lakini wengine wakipinga hatua hiyo.

“Kaka yangu mkubwa alisema asingeweza kukubali kuwa na kaburi la mtu aliyehai, hivyo wote wakakubaliana kuwa mguu wangu uchomwe moto palepale Muhimbili,” alisimulia.

Akiwa anadhani kuwa ‘zimwi’ la mateso limemwacha, siku moja kidole cha kati cha mkono wa kushoto kilianza kuwasha kikiwa na dalili zilezile zilizoonekana kwenye vidole vilivyokatwa hapo awali. Kwa mara nyingine tena alikwenda hospitali ya Kairuki kupatiwa matibabu lakini alitibiwa siku chache kisha akahamishiwa Muhimbili ambako waliamuru kidole hicho kikatwe.

“Baada ya kukatwa tofauti na vidole vingine, hiki kilianza kuoza na kutoa funza kama vile mtu aliyekufa,” alifafanua na kuongeza kuwa: “Nilikuwa nasikia maumivu makali lakini kitu cha ajabu daktari alikuwa ananisafisha bila ganzi, nilimwambia akasema ataniacha asinisafishe nikamwambia ‘niache’ akaniacha.
“Nilichukua njiti ya kiberiti nikaanza kuwatoa wale funza mimi mwenyewe.”

Wakati bado akiwa anaendelea na matibabu ya kidole kilichokatwa, kidole kingine kikaanza kuuma nacho kikiwa na dalili zilezile.

Mwaka 2011 aliamua kwenda Hospitali ya St. Franscis iliyopo Ifakara mkoani Morogoro. Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu waliamua mikono yote miwili ikatwe ili kuzuia maambuzi kuendelea mwili mzima.

“Nikiwa nimebakiwa na mguu mmoja na baadhi ya vidole, wakaamuru mikono yote ikatwe siku moja. Kutokana na maumivu niliyokuwa nayo niliona uamuzi wao ulikuwa sahihi.”

Baada ya kukatwa mikono alikaa hospitali wiki moja kisha akaruhusiwa kwenda nyumbani.
“Nina hofu kuwa wakati wowote huu mguu uliobaki nao utaanza kunisumbua, angalia hapa kwenye hiki kidole cha pili kuna rangi nyeusi inaniogopesha sana kwasababu vingine vyote vilianza hivi hivi,” alisema huku akinionyesha kidole kinachoonekana kimevimba.

Baadhi ya changamoto anazokutana nazo Lombero alisema kila kitu anakifanya analazimika kuomba msaada kutoka kwa mtu aliye karibu naye. Akitaka kula chakula anahitaji mtu wa kumlisha na anapokosekana hulazimika kuinamisha kichwa chake kwenye sahani ya chakula na kuanza kula.
“Siwezi kuoga pekee yangu, ninahitaji mtu wa kunivua nguo na kuniogesha, bahati mbaya mke wangu wakufanya mambo yupo Iringa. Nimeshindwa kukaa naye sina kitu cha kuilisha familia yangu wala fedha ya kulipa kodi,” alieleza kwa mara nyingine tena machozi yanamlenga na kuongeza kuwa:

“Leo asubuhi nilibanwa na haja ndogo, wakati ninahangaika kuiweka nguo sawa...nililowa kidogo. Hivi ndivyo vitu vinavyoniumiza sana, naomba nisaidiwe fedha nikakae karibu na mke wangu.”

Akiongea kwa uchungu anasema: “Kulala na njaa kwangu ni kitu cha kawaida, kuna wakati siogi wiki mbili hata nikitaka kwenda chooni nahitaji mtu wa kunisaidia. Fikiria unataka kwenda chooni halafu kila unayemwambia hataki kukusaidia unafanyaje?” anahoji.

Anasema mara kadhaa alipowatuma watu wamsaidie kununua chakula walikimbia na fedha na kutokomea kusikojulikana huku wengine wakimwibia fedha kwenye M pesa anapokuwa anaomba mtu amsaidie kutoa fedha.

Inaendelea.