KAULI iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda hivi karibuni ya kuruhusu wanaokaidi amri ya polisi wapigwe, imezua taharuki ndani ya Jeshi la Polisi nchini, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Kauli hiyo inayotajwa kuwa ni ya kichochezi, inaonekana kuibua hali ya mshituko ndani ya jeshi, hasa kwa askari wa chini ambao wengi wanaishi uraiani katika nyumba za kupanga.
Taarifa za uhakika kutoka kwa baadhi ya askari wa jeshi hilo zinasema kuwa kauli hiyo imejenga chuki kati yao na raia na imedhoofisha dhana ya Polisi Jamii ambayo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema amekuwa akiisisitiza ili jamii iwaone polisi kama wenzao, hivyo watoe ushirikiano kupunguza uhalifu nchini.
“Hatutaki kuasi, tunapaswa kutii amri za wakubwa, hicho ni kiapo chetu, lakini kauli za aina hii tunashindwa kuelewa Waziri Mkuu alikuwa anakusudia nini, na anatuweka katika mazingira gani, yeye analindwa, sisi tunamlinda.
“Inapotokea kauli kama hii halafu mkaenda kwenye operesheni likatokea la kutokea, mtu kauawa hata kama ni bahati mbaya, ikiundwa tume unabainika ni wewe, hutapata mahali pa kusimama, maana hata tamko hili limetolewa kisiasa.
“Kwa utaratibu huu utajikuta askari mdogo umeshitakiwa katika mahakama ya kijeshi umevuliwa, unarudi uraiani unafungwa milele,” alisema askari mmoja kwa manung’uniko.
Mwengine aliongeza: “Tukirejea tukio lililotokea Lindi, kule Kibiti, Januari mwaka huu, wananchi walijichukulia sheria mkononi, wakachoma makazi ya askari.
“Askari wote wenye nyumba zilichomwa moto na wale wanaoishi katika nyumba za kupanga wananchi wenye hasira waliingia kwa kuchagua vyumba vyao kutoa nje vitu vyao na kuvichoma. Katika tukio hilo, askari wengi sana waliachwa katika hali mbaya.
“Sasa Waziri Mkuu anatuchongea tuonekane kazi yetu ni kupiga tu, badala ya kuelimisha jamii kuacha uhalifu... Hatuna mamlaka ya kumwambia Waziri Mkuu ila kauli hii inaweka rehani mahusiano yetu na jamii.”
Askari mwingine aliyezungumza na gazeti hili, alisema kuwa kila raia anayekataa kutii amri halali ya polisi ukisema apigwe tu, nchi itakuwa inaendeshwa kidikteta na matokeo yake ni uhasama kati ya Jeshi la Polisi na raia.
Taharuki hiyo kutoka ndani ya polisi inakuja baada ya kauli tata ya Waziri Mkuu Pinda aliyoitoa bungeni akiwataka askari kuwapiga wote wanaokaidi amri halali ya polisi, huku akisisitiza kuwa serikali imechoka kuwavumilia.
Akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu bungeni mjini Dodoma wiki hii, Pinda alisema: “Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi, watakupiga tu... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.”
Kauli hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu nchini.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Wakili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, Mabere Marando alisema: “Nimeshangaa kauli ya Pinda, na nia aibu kubwa kwa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na wanasheria wote waliohitimu miaka ya 1970 ambapo kulikuwa na walimu wazuri, hatuna cha kusingizia kuwa hakuelewa sheria.
“Niseme tu kwamba kauli ya Pinda ni kibali kibaya sana kwa vyombo vya dola, na ni uthibitisho kuwa mwenendo wa serikali na polisi kuua kisha kupandishwa vyeo sio bahati mbaya, ila ni msimamo wa serikali.”
Marando alisisitiza kwamba kauli ya Pinda kuwa wamechoka, maana yake hawataki kusikiliza wananchi tena, na anatoa kibali kuwa wananchi wakienda kuuliza au wakiwa na jambo ambalo hawajaelewa, basi wapigwe na viongozi.
“Huu ni ushauri mbaya sana, tena toka kwa Waziri Mkuu wa nchi,” alisema.
|
|
0 Comments