Uganda imetangaza kuweka kodi ya 10% kwa pesa zote zinazotumwa
kwa njia ya simu na mbinu zingine za kutuma pesa.
Hii itaathiri pesa zinazotumwa na Waganda waishio nchi za ng'ambo. Waziri wa fedha Maria Kiwanuka pia amesema kuwa anapanga kukusanya zaidi ya $16.5m (£10.6) kwa kutoza kodi simu zote za kimataifa kutoka nchini humo.
Bi Kiwanuka alilazimika kutafuta mbinu ya kuziba pengo la $214m katika bajeti ya serikali ya Uganda, baada ya wafadhili kupunguza msaada wao kwa Uganda kufuatia madai ya ufisadi.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala , anasema kuwa wengi wanahofia kuwa bajeti hii, iliyosomwa Alhamisi, inawalemea zaidi watu maskini katika jamii.
Waziri Kiwanuka aliambia bunge kuwa zaidi ya $767m zilizokusanywa na serikali mwaka uliopita zilitoka kwa Waganda waishio ngambo.
Kwa mujibu wa gazeti huru nchini Uganda, Daily Monitor, ushuru huo mpya unaotozwa pesa zinazotumwa kwa simu za mkononi utaathiri zaidi ya watumiaji 8.9m wanaotumia mitandao sita ya simu nchini Uganda.
Serikali inahitaji fedha zaidi
Imeripoti pia kuwa serikali inanuia kukusanya takriban $12m kwa mwaka.
Huduma hii ya kutuma pesa kwa njia ya simu ni maarufu sana nchini Uganda ikizingatiwa kuwa raia wengi wa nchi hiyo hawana akaunti za benki.
Huhduma hii hutumiwa kuwatumia jamaa pesa nyumbani au hata kulipia madeni.
0 Comments