Nini kinatokea mtu akikosa usingizi?

Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha wanaume wengi wanaolala kwa muda mfupi huwa na kiwango kidogo cha kichochezi hiki. Utafiti uliochapishwa mwaka 2006 katika jarida la Sleep and Sports Health uliohusisha wazee wa umri wa zaidi ya miaka 50 unashangaza.

“Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi,” anasema Plamen Penev kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, Marekani.
Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi kwa wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo.


 Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.
Matokeo ya uchunguzi huo yalionyesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi.

Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa saa sita.

“Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa picha ya nini kinachotokea mwilini mtu asipopata usingizi wa kutosha.

Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili,” anasema Dk Penev.
Ushauri

Ili kuimarisha kiwango cha kichochezi hiki ni vyema kuepukana na mambo yanayoweza kuingilia usingizi wako.
Kwa mfano, kuzima kompyuta, simu, taa, runinga, redio na kuacha kulala na vikuza sauti masikioni. 

Tengeneza mazingira ya chumba chako yawe na joto la wastani na uende haja ndogo kabla ya kulala. Inafaa kuongeza muda wako wa kulala kwa saa kumi na muhimu kula lishe bora na mazoezi ya wastani.

Kadri unavyopata usingizi ndivyo kiwango chako cha testosterone huongezeka na kuipa uimara  misuli yako ya mwili.

-------------------------------------------------------
MWANANCHI.