Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba 

Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ametangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya wilaya, huku akiwaonya watu wa kada mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa kutokuingilia mikutano hiyo.

Vilevile Jaji Warioba alieleza sababu za Tume hiyo kupendekeza Serikali tatu, huku akisisitiza kuwa suala hilo lilikuwepo tangu siku nyingi na Tume iliamua kupendekeza Serikali tatu kwa kuwa ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuulinda muungano.

Kauli hiyo inaonekana kama kukijibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimependekeza kuwepo kwa Serikali mbili, ikiwa ni siku chache baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Katiba.
Mikutano hiyo inafanyika baada ya Juni 3 mwaka huu, Tume hiyo kutoa rasimu ya Katiba na kusambaza katika vijiji, mitaa na shehia kwa ajili ya kujadiliwa na wananchi, ambao nao watachangia mawazo yao kwa wawakilishi wao waliowachagua kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, inaeleza kuwa mikutano hiyo itaanza Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu na kutakuwa na jumla ya Mabaraza 177, Tanzania Bara 164 na Zanzibar 13.

Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa mapendekezo yake yanapitishwa huku kikitumia wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wakiwemo wa ngazi ya mtaa, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye akiwaeleza wajumbe wa mabaraza ya Katiba jijini Dar es Salaam juzi azma ya chama hicho kuwa na rasimu mbadala.
Wakati CCM wakieleza hayo, Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana leo na kesho katika kikao cha dharura jijini Dar es Salaam ili kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba Mpya.

Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anayemaliza muda wake, Profesa Issa Shivji, Juni 21 mwaka huu alisema kama Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano ikikubaliwa bila mabadiliko makubwa itasababisha kuvunjika kwa Muungano.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema hairuhusiwi kwa makundi, vyama vya siasa au mtu yeyote kuingia katika mabaraza hayo kwa lengo la kushawishi kukubaliwa na maoni ya aina fulani. Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali na gazeti hili, juu ya taarifa zilizopo kwamba baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeandaa rasimu zao kwa lengo la kuwashawishi wajumbe wa mabaraza kupitisha maoni yao.
“Mikutano na Mabaraza ya Katiba siyo ya kupiga kura bali ni kujadili na kutoa hoja ambazo zitakuwa na msingi kwa masilahi ya taifa na siyo kutetea masilahi ya kundi au watu fulani,” alisema Jaji Warioba na kuongeza;

“Hilo la vyama kuandaa rasimu zao kwa lengo la kuingilia utaratibu huu sijalisikia, ila kikubwa ni kwamba si ruhusa kuingilia mchakato huu kwa sababu utafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizopo,” alisema Warioba na kusisitiza; “Wananchi watoe maoni ambayo yatasaidia kuiboresha rasimu iliyotolewa kwa kuweka mbele masilahi ya taifa na kuepuka ubinafsi wa mtu mmojammoja au makundi ya aina yeyote.”

Alisema Tume yake itapokea maoni na mapendekezo yote ambayo yatakuwa na lengo la kuiboresha rasimu ambayo itaweka umoja wa kitaifa na siyo kuwagawa Watanzania.
“Tunazidi kuwaomba wasiishie kutoa maoni na hofu zao, bali wasaidie tume kutoa mapendekezo ambayo yataisaidia tume katika kazi yake ya kuwapatia Watanzania katiba iliyokuwa bora,” alisema.

Akizungumzia sababu za kupendekeza Serikali tatu, Warioba alisema kama wangependekeza Serikali ya mkataba ilikuwa lazima kuvunjwa kwa muungano na kuwepo kwa Serikali mbili ambazo baadaye zingekaa na kuamua kushirikiana ama laa, jambo ambalo lingekuwa gumu.

“Wapo waliotaka Serikali mbili, lakini katika hilo wapo waliosema kuwa Zanzibar wana wimbo wao wa taifa na bendera, pia wamejiunga na OIC na hata Katiba yao inasema kuwa Zanzibar ni nchi, Watanganyika nao wangeanza kuhoji Tanganyika iko wapi,” alisema.
Alisema ndiyo maana walipendekeza Serikali tatu na kwamba kama wangeamua kuvunja muungano operesheni za sheria tulizonazo zingewatenganisha wananchi, kama soko la pamoja, sheria ya ardhi, mwingiliano wa pande mbili, biashara, matibabu na shule.

Alisema Serikali tatu ndiyo suluhisho la kudumisha muungano kuliko Serikali moja au mbili, na kwamba katika kura ya maoni jambo la uwepo wa Serikali tatu linategemea uamuzi wa viongozi.

Akizungumzia idadi ya wajumbe wa mabaraza hayo alisema Tanzania Bara kutakuwa na wajumbe 18,174 na Zanzibar 1159 na kwamba tume itatumia siku 54 kuendesha Mabaraza ya Katiba nchi nzima.
“Tunazidi kuwaomba wasiishie kutoa maoni na hofu zao, bali wasaidie tume kutoa mapendekezo ambayo yataisaidia tume katika kazi yake ya kuwapatia Watanzania katiba iliyokuwa bora,” alisema.

Akizungumzia sababu za kupendekeza Serikali tatu, Warioba alisema kama wangependekeza Serikali ya mkataba ilikuwa lazima kuvunjwa kwa muungano na kuwepo kwa Serikali mbili ambazo baadaye zingekaa na kuamua kushirikiana ama laa, jambo ambalo lingekuwa gumu.

“Wapo waliotaka Serikali mbili, lakini katika hilo wapo waliosema kuwa Zanzibar wana wimbo wao wa taifa na bendera, pia wamejiunga na OIC na hata Katiba yao inasema kuwa Zanzibar ni nchi, Watanganyika nao wangeanza kuhoji Tanganyika iko wapi,” alisema.
Alisema ndiyo maana walipendekeza Serikali tatu na kwamba kama wangeamua kuvunja muungano operesheni za sheria tulizonazo zingewatenganisha wananchi, kama soko la pamoja, sheria ya ardhi, mwingiliano wa pande mbili, biashara, matibabu na shule.

Alisema Serikali tatu ndiyo suluhisho la kudumisha muungano kuliko Serikali moja au mbili, na kwamba katika kura ya maoni jambo la uwepo wa Serikali tatu linategemea uamuzi wa viongozi.

Akizungumzia idadi ya wajumbe wa mabaraza hayo alisema Tanzania Bara kutakuwa na wajumbe 18,174 na Zanzibar 1159 na kwamba tume itatumia siku 54 kuendesha Mabaraza ya Katiba nchi nzima.
“Ili kuweza kufika sehemu zote za nchi, tume imejigawa katika makundi 14 na kila kundi litaendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya wilaya katika Mamlaka za Serikali za mitaa 12 au 13 na mikutano itafanyika kwa siku tatu,” alisema.

Alisema mikutano ya kwanza itafanyika katika mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mara, Kigoma, Tabora, Lindi, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mkoa wa Kusini Unguja, Mbeya, Rukwa, Mtwara na Njombe.

CCM

Tangu rasimu hiyo ilipotolewa mapema Juni mwaka huu, chama hicho kilionyesha kutokuridhishwa na rasimu hiyo na kuahidi kuipeleka kwa wanachama wake.

Katika kuonyesha kutokuridhshwa huko, Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye aliwaeleza wajumbe wa Mabaraza ya Katiba jijini Dar es Salaam juzi azma ya chama hicho kuwa na rasimu mbadala.

Nape ambaye aliitumia siku nzima ya Alhamisi kuzungumza na wajumbe hao wa mabaraza, alisema wameandaa rasimu yao ambayo imeandikwa vitu wanavyohitaji na wanachama wote wanapaswa kuvisimamia.
Alisema ili kurekebisha kasoro hizo CCM kimeandaa rasimu ambayo imetengenezwa katika mazingira ya kisiasa na kitaalamu ambapo haitokuwa mzigo kwa chama hicho.

Alisema katika vitu muhimu ambavyo wanapaswa wajumbe wa chama hicho kuvipigania ni pamoja na suala la Serikali tatu.

Nape alisema kipengele cha Serikali tatu ambacho kinaitwa Serikali ya shirikisho kinapaswa kupiganiwa kifutwe kutokana na nchi kutokufikia hatua ya kuwa shirikisho.

Alisema kitengo cha kuweka Serikali tatu kinaweza kuongeza urasimu pamoja na kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali hizo.
Alisema harakati za kutangaza rasimu ya CCM zinafanyika nchi nzima kwa kutumia makada wa chama hicho katika baadhi ya mikoa ambapo katika Visiwa vya Zanzibar zoezi hilo lilifanyika Julai tatu.

Alisema rasimu hiyo inatarajiwa kwenda kupelekwa katika kikao cha Wajumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) itajadiliwa na wajumbe wote ili kuweza kupata mawazo mengine ya wajumbe.

Chadema nao wakutana

Taarifa iliyotolewa na chama hicho imetaja mambo mengine yatakayojadiliwa kuwa ni pamoja na taarifa ya hali ya siasa nchini, taarifa juu ya mfumo wa uendeshaji wa chama kwa kanda (uzinduzi) na taarifa juu ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 26, uliofanyika Juni 16, 2013.
Kauli ya Shivji

Kauli hiyo ya Shivji aliitoa katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati akitoa mhadhara wa kuaga wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kigoda hicho kwa Wanakigoda wenzake na jumuiya ya chuo hicho.

Profesa Shivji aliainisha upungufu uliomo katika rasimu hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ambapo alisema yanaweza kusababisha kuzuka kwa migogoro mingi na mikubwa itakayovunja Muungano.

Alibainisha rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na thabiti kuhusu ukuu wa Katiba ya Muungano juu ya katiba nyingine za washirika wa Muungano, hali itakayosababisha migongano na kutokuelewana kati ya mamlaka za washirika wa Muungano na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.Alisema kuwa Ibara ya nane ya rasimu hiyo inayozungumzia ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa ina kasoro kubwa kwani imeeleza kuwa ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano tu na si vinginevyo.