Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Iramba Magharibi kwa tiketi ya CCM, Mwigulu Lameck Nchemba ametajwa kuwa baba bora wa familia kufuatia picha yake akiwa na mkewe, watoto watatu, mmoja mgongoni kwake kuanikwa mtandaoni hivi karibuni.Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, katika picha hiyo anaonekana amesimama sebuleni, nyumbani kwake akiwa amembeba kwa mbeleko mtoto wake mdogo huku akiachia tabasamu pana lenye amani.

Mtu aliyetupia picha hiyo alisema mheshimiwa huyo ni baba bora kwani hajaonesha nafasi yake ya kikazi ndani ya familia.
Aliandika hivi: “Mwanasiasa kijana na machachari mheshimiwa  Mwigulu ameonesha mfano wa kuigwa kwa viongozi wote wa vyama na serikali kuhusu suala zima la namna ya kuongoza.
“Mheshimiwa Mwigulu ana amini katika falsafa ya kiongozi bora anaanzia nyumbani jambo ambalo ana imani nalo na analifanya kwa vitendo.
“Kama wewe unasema ni kiongozi na unaweza kuliongoza taifa, ni vyema ukaanza na ngazi ya chini kabisa ambayo ni familia. Familia itatoa matokeo ya namna ambavyo utaweza kuongoza kundi kubwa la watu ama lah!
“Tunao wanasiasa ambao hata familia ziliwashinda kuongoza. Wanasiasa hao wamekuwa wanakimbia familia zao na kuacha watoto wao wakiwa wanatangatanga.
“Wanasiasa wote walioasi familia zao na kuzikimbia hawafai kupewa nafasi ya kuongoza kundi kubwa la watu, kwa kuwa tayari wameshaonesha udhaifu katika kuongoza kwenye ngazi ya chini kabisa ambayo ni familia”
Akaendelea: “Rai yangu,
familia iwe kipimo cha mtu kupata madaraka, kuna haja ya kuliweka hili kama moja ya vigezo vya mtu kupata uongozi hasa kwenye zile nafasi za kimaamuzi ndani ya chama na hata serikalini ili isaidie hata katika kumpima mtu uwezo wake wa kiuongozi katika ngazi ya awali kabisa ambayo ni familia.”
Hata hivyo, wengine walimponda mtu huyo kwa kuandika maoni yaliyoashiria hasira badala ya hoja.

GPL