Wake wa viongozi Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, wameiomba serikali kuitazama kesi inayowakabili viongozi hao kwa jicho la uadilifu, haki na sheria ili kuonesha dhana ya utawala bora.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kongamano la wanawake wa Kiislamu lililofanyika msikiti wa Mbuyuni, kinamama hao wamelalamikia  kesi hiyo kuchukua muda mrefu huku ikiwa hakuna hatua yoyote muhimu inayochukuliwa ili haki itendeke.
Wametaka vyombo vya sheria vifanye kazi kwa maadili, hasa ikizingatiwa kwamba  Zanzibar ni mshiriki wa Muungano wa Tanzania ambayo ni mwanachama wa taasisi mbalimbali za kulinda na kuheshimu haki za binadamu ulimwenguni.
“Hatukusudii kuingilia kazi za mahakama, bali tunaeleza hali halisi ya uvunjwaji wa sheria na katiba ya nchi kwa vyombo vya sheria kufanya kazi kwa utashi bila ya kuzingatia haki za wanachi mbele ya sheria”, walidai wanawake hao.
Walidai kuwa, kitendo cha kunyima haki kinaweza kuitia doa kubwa mahakama na serikali mbele ya macho ya kimataifa.
Aidha, walitaja sababu za kuwekwa ndani waume zao kuwa ni harakati zakuongoza umma wa Wazanzibar kudai haki yao ya msingi juu ya hatima ya Zanzibar kuwa nchi yenye uhuru wa kujiamulia mambo yake.
Wameeleza kusikitishwa kwao kwa kusema kuwekwa ndani kwa waangalizi hao wa familia zao, kumewaathiri sana kisaikolojia na kiuchumi.
Pia wamesema mwenendo mzima wa taaluma za Kiislamu ambazo viongozi hao walikuwa wakifundisha katika madarsa mbalimbali kwenye misikitini na vyuo, umeathiriwa na kushikiliwa kwa viongozi hao.
Kwa hivyo wamevitaka vyombo vya sheria kufanya haki katika maamuzi yao ili kudumisha amani na utulivu uliopo pasi na kutia dosari serikali ya umoja wa kitaifa iliyowalea Wazanzibari pamoja.
Kupitia kongamano hilo, wanawake hao wameviomba vyombo vya sheria, kuwaruhusu viongozi hao kuonana na wake na ndugu zao wakati wanapofikishwa mahakamani kwa kusikilizwa kesi yao.
Katika hatua nyengine, kinamama hao  wameunda kamati ya kufuatilia na kuratibu mwenendo wa kesi pamoja na kuonana na watendaji wa haki za binadamu.