Dk Shukuru Kawambwa 
 
Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mboka Mwambusi ameitaka Serikali kupanga upya alama za ufaulu ili kumaliza tatizo la pengo la wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano.

Mwambusi alisema jana kuwa kiwango cha chini cha ufaulu kinachotumika sasa kwa wanafunzi wa kidato cha nne cha shule za sekondari kinamtaka mwanafunzi awe angalau na alama tatu za C ndipo achaguliwe jambo ambalo alisema ni gumu kwa wanafunzi wengi.

“Kiwango hicho kimekuwa ni kikwazo hasa ukilinganisha na kiwango cha alama cha D ambazo vyuo vingi vimekuwa vikitumia kuruhusu wanafunzi kujiunga na masomo ngazi ya cheti ya fani mbalimbali. Baada ya hapo wanatoa nafasi kwa wanafunzi hao kuendelea na masomo ya stashahada kabla ya kujiunga na vyuo vikuu,” alisema Mwambusi.
Alisema hali hiyo ni tishio kwa shule za sekondari zinazotoa elimu ya kidato cha tano na sita, hasa kwa kuwa imeonyesha wanafunzi wengi wamekuwa wakivutiwa kujiunga na vyuo kuliko kuhangaika kusaka alama za ufaulu wa kujiunga na kidato cha tano na sita.

“Nasema ni tishio kwa kuwa mwanafunzi anayejiunga na chuo moja kwa moja anakuwa anasomea taaluma (fani) husika hivyo hapotezi muda, bali anajijengea mazingira mazuri katika fani anayoipenda, nafikiri inaweza kufika wakati wamiliki wengi wakaamua kufungua vyuo,” alisema.
Mwambusi alilipongeza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), kwa kuweka utaratibu huo ambao umewezesha vijana wengi kujiunga na elimu ya juu.

Alipongeza pia hatua ya gazeti hili kuandika habari juu ya kuchelewa kutangazwa kwa wanafunzi wanaojiunga na masomo ya kidato cha tano, habari ambayo iliishtua Serikali na kutangaza majina hayo juzi. 

“Habari ile imetusaidia wanafunzi, wamiliki wa shule, walimu na wazazi kwa ujumla wengi tulikuwa gizani lakini taarifa ile iliizindua hata Serikali,” alisema Mwambusi.