Watu watano wameuawa kwenye shambulio la bomu la kujilipua, lililolenga wanajeshi wa kutunza amani wa Muungano wa Afrika mjini Mogadishu, Somalia.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, ameiambia BBC kuwa ameona miili ya raia watano, ambao walikufa baada ya bomu hilo lililokuwa ndani ya gari kulipuka.
Muungano wa Afrika umethibitisha kuwa wanajeshi wake wawili walijeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo la Bomu, lakini kundi la Al shabaab lililo na uhusiano na kundi la kigaidi ya Al-Qaeda limewahi kufanya mashambulio kama hayo mjini Mogadishu.
Kundi hilo la Al-Shabab, linataka kuundwa kwa taifa la Kiislamu la Somalia, licha ya kuwa wapiganaji wake wametimuliwa kutoka mji mkuu wa nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Al Shabaab bado linadhibiti maeneo kadhaa ya Somalia.
Zaidi ya wanajeshi elfu kumi na nane wa Muungano wa Afrika wako nchini Somalia, kuisaidia serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na rais Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alichaguliwa na wabunge September mwaka uliopita