KAULI ZA KISIASA
 Hivi karibuni mnamo tarehe 21/09/2013 vyama vya siasa kadhaa vilifanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani, Pamoja na mambo mengine yaliyo zungumzwa, mimi kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nimestushwa na baadhi ya ujumbe wa maneno uliopelekwa kwa wananchi. Ambao unaweza kuleta madhara kwa jamii, hususan wanawake, watoto, wazee, walemavu n.k.
                       
Kwanza, Kauli ya Mhe. Lipumba

Mheshimiwa huyu kati ya maneno yote aliyoyasema pale Jangwani, nadhani jamii inahitaji kutafakari na kuhoji; maana ya kauli yake aliposema, “Vijana msikubali wakati wa kufanya mazoezi umefika” Tujiulize, Je, ni mazoezi ya aina gani? Yanafanyikia wapi? Yanalenga kufanya nini? Lakini mwisho wa yote ni muhimu Watanzania wakajikumbusha mwenendo wa siku za nyuma za hao wanaoitwa vijana wake!

Wito wangu kwa vijana wasikubali kutumiwa katika mambo yanayo wahatarisha wao na jamii kwa ujumla, kwani hayana tija. Wananchi kumbukeni kuwa yanapotokea matatizo, akina mama ndio walezi wa majeruhi, wagonjwa na pia walezi wa watoto wa walioathirika.

Pili, Kauli ya Mhe. Mbowe

Mheshimiwa huyu kati ya maneno yote aliyoyasema, nilipatwa na butwaa kwa kauli yake aliposema:- “Siku ya tarehe 10/10/2013 ni Siku Maalum ya Kitaifa ya “Civil Disobedience”. Hii ni kauli hatari, yenye kuashiria uwepo wa njama mbaya za kuwashawishi wananchi ili siku hiyo wajichukulie sheria mkononi, kinyume cha katiba, sheria na haki za binadamu.


Tujiulize “Siku Maalum ya Kitaifa ya Civil Disobedience” maana yake nini? Kwa Kiswahili maana yake ni Siku Maalum yaKitaifa ya Jamii Kutotii, kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa. Hayo yakitokea itakuwa ni Siku ya Maangamizi. JAMII KUTOTII ni utovu wa Nidhamu, ambao husababisha Uvunjaji wa Sheria na kuhamasisha kujenga Mazingira ya Vurugu.
Kwa nafasi yangu kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nasema hii ni hatari. Na athari zake naziona kubwa kwa wanawake, watoto, walemavu na wazee.

Tatu, Kauli ya Mhe. Mbatia
Mheshimiwa huyu kati ya maneno yote aliyoyasema, nadhani jamii inahitaji kutafakari na kumpongeza kwa kauli yake aliposema:- Bado anaamini kwamba “Kuna fursa ya kukaa katika round table na kuyazungumza”. Hii kauli ni ya kizalendo na ya kiungwana. Nampongeza sana. Inavyoonekana, Mhe. Mbatia ni mtu mwenye kutambua kwamba ana dhamana ya kuilinda familia yake na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Tahadhari ya kauli zenye kuashiria uvunjifu wa sheria na tabia za vurugu katika jamii
Mwenendo wa kauli hizi, si mzuri kwa maendeleo na ustawi wa jamii yetu kijamii na kiuchumi. Hii ina maana siku hiyo ya Civil Disobedience, Mama Lishe na Wajasiriamali wengine hawatofanya biashara zao, watoto wetu hawatoenda shule na huduma nyingine za kijamii zitakwama wakati wao wakitekeleza mipango waliyopanga kwa tarehe hiyo.
Amani na usalama ni mtaji wa maendeleo
Kama jamii tunapaswa kutambua kwamba amani na usalama, ndio mtaji namba moja wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kidemokrasia. Ustawi wetu kama jamii ya Watanzania au kama familia au mtu mmoja mmoja unahitaji uwepo wa amani, utulivu na usalama. Kwa sababu kunapotokea vurugu/Civil Disobedience wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto, wazee na walemavu.Leo nimeona niongelee hili ambalo linawagusa wadau wangu moja kwa moja ambao wapo chini ya Wizara yangu.

Asanteni.