Na Mwandishi Wetu:
Kwa tathmini ya kile kilichotokea  kati ya Septemba 21 hadi 24, mwaka huu Nairobi, Kenya ambapo magaidi wa Al-Shabaab walivamia maduka makubwa ya Westgate na kuua watu 69 kisha kujeruhi wengine 175, hali si shwari jijini Dar, Tanzania na hofu imetanda maeneo yenye watu wengi kama Mlimani City watu wakijiuliza who’s next? Nani anafuata?AL- SHAABAB WALIANZIA UGANDA
Kabla ya tukio la Nairobi, kumbukumbu zinaonesha kwamba tukio lingine baya kama hilo, liliwahi kutokea jijini Kampala, Uganda Julai 11, 2010 na kusababisha vifo vya watu 76.
Katika tukio la Uganda, Al-Shaabab walikiri kuhusika na mashambulio mawili yaliyotokea siku hiyo; la kwanza likiwa ni kwenye mgahawa unaotembelewa na watalii wengi wa Ethiopian Village, Kabalagala jijini humo.
Muda mfupi baadaye, milipuko miwili ilitokea kwenye Ukumbi wa Kyadondo Rugby, Nakawa ambako fainali za Kombe la Dunia 2010 zilikuwa zikioneshwa kati ya timu za Uholanzi (Netherland) na Hispania (Spain).MAENEO HATARI TANZANIA
Uchunguzi umeonesha kwamba kwa kuangalia mashambulio ya Nairobi na Uganda, Al- Shabaab wanalenga zaidi maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi ambapo kwa Dar es Salaam, Mlimani City, Stendi ya Mabasi ya Mikoani Ubungo, Quality Centre, Kariakoo sokoni, Kivuko cha Feri, ndani ya Treni ya Mwakyembe, Mkapa Tower (Posta) na kwenye viwanja mbalimbali vya mpira ambako Ligi Kuu  Bara inaendelea yanatajwa kuwa hatari.UJUMBE WASAMBAZWA
Katikati ya wiki hii, ujumbe mfupi wa maneno ‘SMS’ unaotahadharisha juu ya kutokea kwa mashambulio ya kigaidi Dar es Salaam unaodaiwa kutolewa na kundi la Al-Shabaab ulianza kusambazwa.
Kwa mujibu wa watu waliopata ujumbe huo wa aina mbili, vyombo vya usalama vya Tanzania, viyaangalie maeneo tajwa.
Ujumbe wa kwanza ulisomeka: “Al-Shabaab wanahisi Tanzania ina ushawishi au inaunga mkono kitendo cha Kenya kupeleka makundi ya wanajeshi nchini kwao, Somalia.
“Kama Kenya haitaondoa majeshi yake Somalia hadi Septemba 27, mwaka huu, Tanzania itakumbwa na tukio la kigaidi kati ya Septemba 28 (leo) na 29, maeneo yanayolengwa ni Mlimani City na Quality Centre, Dar. Tuma ujumbe huu kwa wengine wote ili wakae majumbani kwa usalama wao.”
Ujumbe mwingine unaodaiwa kusambazwa na kundi hilo ulisomeka: “Tumevamia Kenya kwa sababu waliwahi kutuvamia tukiwa kwetu Somalia. Tumefanya hivi kulipa kisasi, tutavamia pia Tanzania na Uganda muda wowote.”
HOFU YATANDA
Meseji hizo ndizo zilizosababisha hofu kubwa jijini Dar juu ya Al-Shabaab ambapo kwa sasa watu wanakwepa kutembelea baadhi ya maeneo yenye mikusanyiko mikubwa yasije yakatokea mauaji kama Kenya ambapo watu 69 waliuawa.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa katika maeneo hayo, kwa mfano Mlimani City, hakuna vyombo vya ukaguzi imara wa watu wanaoingia getini na kutoka hivyo Al-Shabaab wanaweza kuingia na silaha kiulaini na kuua watu watakavyotaka.WALINZI WA MLIMANI CITY
Ilibainika kuwa walinzi wamekuwa wakikagua magari kwa nje tu na kutoa kadi za kuingilia bila kujua ndani ya magari hayo kuna kitu gani.
Pia ilibainika kwamba walinzi waliopo wanalinda zaidi magari kuliko watu, jambo ambalo ni hatari na matokeo yake watu wameanza kukauka maeneo hayo katika kipindi hiki cha hofu ya mashambulio kutoka Al-Shabaab.
Kwa kawaida, watu wanaoingia maeneo kama Mlimani City, wanapaswa kukaguliwa kwa mashine maalum ya kutambua kama mtu ana silaha, jambo ambalo halifanyiki.
CHONDECHONDE IGP
Risasi Jumamosi linatahadharisha na kuliomba Jeshi la Polisi Tanzania chini ya IGP Said Mwema kuhakikisha ulinzi unaimarishwa maeneo yote nchi nzima na si Mlimani City na Quality Centre pekee.