Na Fredy Azzah, Mwananchi
Mtoto wa miaka minne ambaye ni raia wa Uingereza, Elliott Prior ameonyesha ushujaa wa hali ya juu baada ya kuweza kuwatolea maneno makali na ya kugusa magaidi waliovamia jengo la maduka la Westgate.
Baada ya maneno hayo, baadhi ya taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya kimataifa, vinasema magaidi hao waliomba mtoto huyo awasamehe kwa maelezo kuwa wao siyo watu wabaya.
Inaelezwa kuwa, kitendo cha mtoto huyo kilikuwa cha kishujaa kwani aliweza kuwaeleza magaidi hao maneno hayo, bila kuogopa silaha nzito walizokuwa wameshika mkononi huku baadhi ya watu wakiwa wameshauuawa.
Mtandao wa Daily Mail unasema mtoto huyo alimwambia mmoja wa magaini hao kuwa ‘Nyie ni watu wabaya sana’.
Mtandao huo unasema mtoto huyo aliyasema maneno hayo kama njia ya kumkinga mama yake Amber, aliyekuwa amepigwa risasi mguuni pamoja na dada yake Amelie, mwenye umri wa miaka sita ambaye walikuwa wote ndani ya duka hilo.
Katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni kuumizwa na maneno hayo, magaidi hao walimpa Elliott pamoja na dada yake mifuko miwili miwili ya chokleti na kuwaomba msamaha.
Taarifa hizo zinasema kuwa,  gaidi huyo alisema “Samahani nisamehe, sisi siyo watu wabaya”.
Mama huyo anasema kuwa, kabla ya kukamatwa na magaidi hao, yeye na watoto wake walikuwa wamejificha kwenye jokofu la kuhifadhi nyama lililopo ndani ya duka la Nakumatt kwa zaidi ya saa moja na  nusu.
Anasema kuwa, baada ya kukamatwa na magaidi hayo, walimpiga risasi ya paja.
Mjomba wa watoto hao aliliambia gazeti la The Sun la Uingereza kuwa  “Walikuwa na bahati kuweza kutoka kwenye mikono ya hao magaidi. Hao magaidi walisema kuwa, kama kuna mtoto yeyote aliye hai ndani ya jengo hilo wanaweza kuondoka.
‘Mama yao alisimama na kusema ‘ndio’ , binamu yangu aliweza kupata ujasiri wa kusimama na kuwaambia kuwa, nyie ni watu wabaya sana’.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, baada ya magaidi hao kujua kuwa mama huyo na watoto wake hawakuwa kati ya watu waliowalenga, hawakuwaua.Mama huyo anasema baada ya kuwaachia  walimshawishi yeye na watoto wake kujiunga na dini ya Kiislamu wakidai kuwa, imani ya dini ya Kiisilamu haina ubaya wowote.
 “Aliniambia natakiwa kubadili dini niwe Muislamu, na akaniuliza ‘unatusamehe,  unatusamehe)” mama huyo aliliambia gazeti la Independent la Uingereza.
“Kwa kawaida ningesema tu chochote walichotaka ili watuachie tuondoke,” anasema mama huyo.
Baadaye magaidi hao waliwaruhusu watoto hao kutoka nje ya jengo hilo wakiwa na watoto wengine wawili akiwamo mmoja mwenye umri wa miaka 12 ambaye awali alikuwa akikataa kutoka, aking’ang’ania kwenye mwili wa mama yake ambaye alikuwa ameshafariki.
Mama wa mtoto Elliott anasema kuwa, walifanikiwa kutoka kwenye mikono ya magaidi hao kimiujiza.
Anasema kuwa, pamoja na vitu vingine walifika kwenye duka hilo ili wakanunue maziwa.
Amber anasema kuwa, magaidi hao waliwaeleza kuwa lengo lao ni kutaka kuwaua raia wa Kenya na wale wa Marekani tu.
Baadaye watoto hao walikuja kuonekana nje ya jengo hilo wakiwa wameshikilia chokleti ambazo wanadaiwa kupewa na magaidi hao, huku pembeni yao kukiwa na mwili wa mtu aliyefariki dunia.
Baba wa mtoto huyo, anasema kupona kwa familia yake kwenye tukio hilo ambalo magaidi hao waliua zaidi ya watu 62, ni muujiza wa aina yake.
“Nashukuru sana familia yangu iko salama, nilidhani watakuwa miongoni mwa wale ambao hawakuwa na bahati,’’ Prior  alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari.
‘‘Kwa sasa kama familia tunataka muda kidogo na faragha, lakini tunaomba sana wale wanaotaka kusaidia majeruhi wa tukio hili huko Kenya, watoe msaada wao kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya,” alisema.