Moja ya magofu ya nyumba yaliyobakia katika eneo la Saadani. Picha na Charles Kayoka. 
Kama unasafiri kwenda Sadani, mji maarufu wa kihistoria, kwa ajili ya kujionea nini kimebaki katika historia hiyo (nikimaanisha majengo, kama sehemu ya ushahidi), nakwambia utabwaga moyo wako mara ukifika pale. Ni kwa muda mrefu nimekuwa na shauku ya kwenda  huko ili kuandika historia ya Saadani.
Waandishi maarufu wa zamani hasa  mpelelezi wa Kiingereza, Sir Francis Burton katika miaka ya 1860-1980 waliiandika Saadani kama mji uliokuwa na ustawi mkubwa wa ustaarabu wa Kiswahili (pwani) ulioathiriwa kwa kiasi kikubwa na utamaduni wa Kiarabu, biashara ya meno ya tembo, chumvi na gundi.
Saadani ilizungumziwa kama kituo kikubwa cha kibiashara  katika karne ya 19, lakini hiyo Saadani ya kihistoria inashuhudiwa na mti mkubwa wa Mbuyu Kinyonga, ambao kama usipoambiwa na wenyeji ambao walikuwa watumwa, huwezi kujua kama ilikwa ni eneo maarufu.
Mti huu umezeeka, lakini hakuna hata kibao kinachosema mti huo una uhusiano gani na historia. Msikiti wa kale uliokuwapo tangu wakati huo umejengwa upya, na kwa sababu ya kukosa ushirikishwaji wa wataalamu, umekarabatiwa kwa ujenzi wa kisasa, na kupoteza kila kitu kinachohusiana na historia yake kiujenzi.
Jirani na kuna ukuta mmoja mrefu ambao una madirisha. ‘Hii ilikuwa jamatini ya wahindi,’ alitueleza mkazi mmoja, lakini zaidi ya ukuta huo mmoja ambao umebaki, hakuna ushahidi zaidi. Yule mkazi aliendelea kutuonyesha mahali kama mita kumi na tano kutoka pale tulipokuwa, ‘pale palikuwa na nyumba ya ghorofa moja iliyojengwa kutoka wakati huo, lakini imebomolewa kwa kukosa matunzo badala yake wakazi wa hapo walijenga makazi ya kawaida na historia imefutika. Hatujui tena nyumba hiyo ilikuwaje,’ anabainisha
Mengine yenye ushahidi wa kihistoria ni kiwanja cha makaburi ya Wajerumani, kiwanja ambacho nina uhakika Barabara ya Tanga-Bagamoyo ikijengwa  makaburi hayo yatabomolewa.
Nasikia kuna kaburi la askari aliyempiga risasi muasi Bushiri, lakini sikulitambua ni lipi. Kuna makaburi mawili tu yenye majina, na mengine yapo yapo tu.
Ckayoka28@yahoo.com, 0766959349