Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe PICHA|MAKTABA

Hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete na kuzungumzia kwa undani mchakato wa Katiba Mpya, imeacha maswali mengi huku ikiashiria kutokuwapo kwa mawasiliano madhubuti ndani ya Serikali kuhusu suala hilo.

Kadhalika, hotuba hiyo imeibua mambo mawili ambayo ni hofu ya kuahirishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba na kuzidi kwa lawama dhidi ya wabunge wa CCM pamoja na uongozi wa Bunge, hususan Naibu Spika, Job Ndugai.

Itakumbukwa kuwa mara baada ya muswada wa awali kupitishwa, baadhi ya mawaziri walinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakisema kusingekuwapo na mwanya kwa Rais Kikwete kukutana na wapinzani kwani upitishwaji wa sheria hiyo ulifuata taratibu zote za kibunge.
Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake ya Septemba mwaka huu kwa taifa, alitangaza kuwapo fursa ya majadiliano baina ya Serikali na viongozi wa vyama vya upinzani; Chadema, CUF na NCCR Mageuzi ambavyo tayari vilikuwa vimeungana kupinga mchakato huo.

Viongozi wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR Mageuzi) walichukua hatua ya kuhamasisha umma kutokubaliana na mchakato huo, wakirejea kutoridhika na jinsi Bunge lilivyoshughulikia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. 
Kauli ya Rais Kikwete kuwaalika wapinzani kwenye meza ya mazungumzo, inatafsiriwa na baadhi ya wasomi kuwa ni aibu kwa Bunge na wabunge waliopitisha sheria hiyo na kwamba ni dhahiri kwamba itarejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Mwanza, Steven Dasu alisema Rais Kikwete ameridhia kuzungumza na wapinzani baada ya kubaini kuwapo udhaifu katika mchakato wa kupitisha sheria husika bungeni na kwamba hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa Katiba yenye tija kwa nchi.

Hata hivyo, Ndugai jana alitetea uongozi wake bungeni huku akisema: “Bunge limefanya kazi yake, inawezekana liliamua vibaya au liliamua vizuri lakini uamuzi ulifanyika. Sasa kama sheria iliyopitishwa ina kasoro inaweza kurekebishwa tu kulingana na taratibu zilizopo”.

Pia aliwaponda wapinzani kwa kile alichokiita kuwa ni kukimbilia kwa Rais, badala ya kujenga hoja zao ndani ya Bunge na kwamba lazima watambue kuwa tabia hiyo haitawapeleka mbali.

 

Lawama kwa wabunge

Wakili wa kujitegemea, Dk Rugemeleza Nshala alisema wabunge hawakuwa makini na kwamba miswada inayotungwa na Bunge kurudishwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuanza kutumika “ni aibu kwa mhimili huo”.

ITAENDELEA